
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA. Anthony Kasore, amesema ujuzi ndio msingi wa utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 kwa kuwawezesha wananchi kushiriki katika uzalishaji wa mali, bidhaa na huduma.
CPA. Kasore amesema hayo jana tarehe 23 Agosti, 2026 katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, akisema maadhimisho hayo yanatoa fursa kwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuwaelimisha wananchi kuhusu kazi na fursa zilizopo.
“Ili taifa liweze kuzalisha mali, bidhaa na huduma, wananchi lazima wawe na ujuzi na uwezo wa kufanya shughuli hizo,” amesema.
Kwa mujibu wa CPA. Kasore VETA ina takribani vyuo 80 katika mikoa na wilaya mbalimbali, huku Serikali ikiendelea kuwezesha ujenzi wa vyuo zaidi kwa lengo la kuhakikisha kila wilaya inakuwa na chuo cha ufundi stadi.
Amesema hatua hiyo itasaidia kusogeza mafunzo karibu na wananchi, kuwawezesha kujiajiri, kuajiri wengine na kuongeza kipato
“Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kupata ujuzi,” amesema, akiwataka wananchi, wazazi, walimu na vijana kutumia fursa za mafunzo zinazotolewa na VETA.
Aidha, amesema kipindi hiki VETA inaendelea kupokea maombi ya wanafunzi wanaotaka kujiunga na mafunzo ya muda mrefu yanayoanza Januari 2027 na kwamba waombaji wanaweza kufanya hivyo mtandaoni au kufika katika vyuo vya VETA vilivyo karibu nao.
Amesema wanafunzi wanaosoma mafunzo ya kutwa hulipa Shilingi 60,000 kwa mwaka, huku wanaosoma kwa mfumo wa bweni wakilipa Shilingi 120,000 kwa mwaka.









