Home Kitaifa NANE NANE 2026: WAJASIRIAMALI WAFURAHIA ELIMU YA TBS KANDA YA KATI, WASEMA...

NANE NANE 2026: WAJASIRIAMALI WAFURAHIA ELIMU YA TBS KANDA YA KATI, WASEMA IMEWAPA MWANGA MPYA

 Na Mwandishi Wetu.

LINDI — Wajasiriamali na wananchi wanaoshiriki Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini wamepata fursa ya kupata elimu muhimu kuhusu ubora wa bidhaa, uthibitishaji na umuhimu wa kuwa na Alama ya Ubora ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hatua inayolenga kuongeza uaminifu wa bidhaa za Tanzania na kufungua fursa zaidi za masoko ndani na nje ya nchi.

Elimu hiyo imetolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Kusini kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini yaliyofanyika katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi, ambapo wananchi na wajasiriamali wamepata fursa ya kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu viwango na ubora wa bidhaa wanazozalisha.

Akizungumza katika viwanja hivyo, Meneja wa TBS Kanda ya Kusini, Bw. Abel Mwakasonda, amesema ushiriki wa TBS katika maonesho hayo ni sehemu ya jitihada za shirika hilo kuwafikia wananchi na kuwapatia elimu inayoweza kuwasaidia kuboresha bidhaa zao na kuongeza ushindani katika masoko.

Amesema TBS imeendelea kuweka mkazo katika kuhakikisha wazalishaji, hususan wajasiriamali wadogo na wa kati, wanaelewa umuhimu wa kuthibitisha bidhaa zao na kuhakikisha zinapata Alama ya Ubora, ambayo ni moja ya nyenzo muhimu katika kujenga uaminifu wa mlaji.

Kwa mujibu wa Mwakasonda, bidhaa yenye kuthibitishwa ubora huwa na nafasi nzuri zaidi ya kuaminika na walaji, jambo ambalo pia humsaidia mzalishaji kujenga soko na kuongeza fursa za kibiashara.

“Tunawakaribisha wajasiriamali na Watanzania kwa ujumla kufika katika banda la TBS ili kupata elimu mbalimbali zinazohusiana na viwango, ubora wa bidhaa na huduma tunazozitoa. Pia tunatoa huduma za usajili wa majengo na huduma nyingine zinazohusiana na majukumu ya TBS,” amesema Mwakasonda.

Amesisitiza kuwa wajasiriamali hawapaswi kuona uthibitishaji wa bidhaa kama kikwazo, bali wanapaswa kuuchukulia kama fursa ya kukuza biashara zao, kuongeza thamani ya bidhaa na kupata imani ya walaji.

Aidha, amewakumbusha wajasiriamali kuwa uthibitishaji wa bidhaa na upatikanaji wa Alama ya Ubora kwa wajasiriamali unaotolewa kupitia utaratibu wa Serikali ni bure, hivyo amewataka kutumia fursa hiyo kuboresha bidhaa zao na kuongeza ushindani katika soko.

Kwa upande wa wajasiriamali walioshiriki maonesho hayo, elimu inayotolewa na TBS imeelezwa kuwa ni muhimu katika kuwasaidia kuelewa namna ya kuboresha bidhaa zao na kuzifikisha katika masoko yenye ushindani.

Bi. Khadija, mchakataji wa bidhaa za mwani, amesema elimu hiyo imempa uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kufuata viwango na kuthibitisha bidhaa, akieleza kuwa hatua hiyo inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kukuza biashara yake.

Amesema awali baadhi ya wajasiriamali wamekuwa wakijikita zaidi katika uzalishaji bila kutambua kwa kina umuhimu wa ubora, ufungashaji, taarifa sahihi za bidhaa na uthibitishaji, lakini elimu inayotolewa na TBS imewapa mwanga mpya wa namna ya kuifanya bidhaa yao iwe tayari kushindana katika masoko mapana.

“Elimu hii imenisaidia kuelewa zaidi umuhimu wa kuthibitisha bidhaa ninazozalisha. Nimepata uelewa kwamba Alama ya Ubora inaongeza imani kwa mteja na inaweza kusaidia bidhaa yangu kufikia masoko makubwa zaidi,” amesema Bi. Khadija.

Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kusini umeifanya taasisi hiyo kuwa sehemu muhimu ya utoaji wa elimu kwa wananchi, huku banda lake likitumika kama kituo cha maarifa kwa wajasiriamali wanaotaka kujua zaidi kuhusu viwango, ubora na taratibu mbalimbali zinazohusiana na bidhaa na huduma.

Katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kusisitiza uzalishaji wenye tija, kuongeza thamani ya mazao na kukuza bidhaa zinazoweza kushindana katika masoko ya kimataifa, elimu hiyo inatajwa kuwa muhimu kwa wajasiriamali wa Kanda ya Kusini na Tanzania kwa ujumla.

Kwa wajasiriamali, Alama ya Ubora si nembo tu kwenye kifungashio cha bidhaa, bali ni ishara inayoweza kujenga imani ya mlaji, kuongeza ushindani na kufungua milango ya masoko mapya.

Kupitia ushiriki wake katika Nane Nane, TBS Kanda ya Kusini imeendelea kuonyesha kuwa jukumu la kuhakikisha bidhaa zinafikia viwango halikomei katika ukaguzi pekee, bali linaenda sambamba na kutoa elimu, kuwawezesha wazalishaji na kuwajengea uwezo wa kushindana katika uchumi unaozidi kuwa wa ushindani.

Hivyo, wajasiriamali na wananchi wametakiwa kutumia fursa ya maonesho hayo kufika katika banda la TBS, kupata elimu, kuuliza maswali na kujifunza hatua wanazoweza kuchukua ili bidhaa zao ziwe na ubora unaokubalika na kuwa na nafasi kubwa zaidi katika masoko ya ndani na nje ya Tanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!