
Na Magrethy Katengu–Mzawa Media
Dar es salaam
Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) linatarajia kufanya Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuanzia Oktoba 20 hadi 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, likiwakutanisha zaidi ya washiriki 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari Leo Juni 12,2026 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Jasper Makala, amesema jukwaa hilo linaandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kwa lengo la kujadili mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Makala amesema jukwaa la mwaka huu litabeba kaulimbiu isemayo, “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Uwazi na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza mashirika hayo kutumia mbinu bunifu katika utekelezaji wa shughuli zake, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza uwezo wa kujitegemea kifedha.
Ameeleza kuwa jukwaa hilo litawakutanisha wanachama wa mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari na wadau wengine muhimu kwa lengo la kujadili mustakabali wa sekta hiyo pamoja na mchango wake katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Aidha, mijadala mbalimbali itafanyika ikijikita katika namna mashirika yasiyo ya kiserikali yanavyoweza kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, kuimarisha vyanzo vya ndani vya fedha, kutumia teknolojia na ubunifu, pamoja na kuendeleza misingi ya uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yake.
Baraza hilo limewataka wadau wote wa maendeleo, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla kujitokeza kushiriki kikamilifu katika jukwaa hilo muhimu, likisisitiza kuwa sekta hiyo ina nafasi kubwa katika kusaidia juhudi za serikali za kuboresha maisha ya wananchi kupitia elimu, afya, uchumi na huduma nyingine za kijamii.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NaCoNGO, Fransica Mboya, amesema kupitia ushirikiano huo mpana wanatarajia kupata maazimio na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mazingira wezeshi ya utendaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, kuongeza ushirikiano wa kimkakati baina ya wadau mbalimbali na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.









