Home Kitaifa WATAALAMU WA AFYA NCHINI WATAKIWA KUWA MFANO BORA KATIKA JAMII

WATAALAMU WA AFYA NCHINI WATAKIWA KUWA MFANO BORA KATIKA JAMII

Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya dawa na vifaa tiba Bw. Emmanuel Tayari akizumgumza kwenye Kongamano la kisayansi la madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mkutano mkuu wa chama leo Mei 29,2026 Jijini Dodoma.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha madaktari wa magonjwa ya ndani Tanzania (APHYTA), Dkt. Kajiru Kilonzo akizumgumza kwenye Kongamano la kisayansi la madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mkutano mkuu wa chama leo Mei 29,2026 Jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la kisayansi la madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mkutano mkuu wa chama leo Mei 29,2026 Jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu- Dodoma

Wataalamu wa afya nchini wametakiwa kurejesha nafasi yao kama mfano bora katika jamii kwa kuwalea, kuwahamasisha na kuwaandaa kitaaluma madaktari na wataalamu wapya ili kujenga mfumo imara wa huduma za afya nchini.

Rai hiyo imetolewa leo Mei 29,2026 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya dawa na vifaa tiba Bw. Emmanuel Tayari kwenye Kongamano la kisayansi la madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na mkutano mkuu wa chama linalofanyika kwa siku mbili na kubeba Kauli mbiu isemayo, Linda Maisha ya Baadaye kwa Kuimarisha Huduma za Afya Kupitia Tiba Kinga.

Bw. Tayari ameeleza kuwa jamii imekuwa ikikosa mifano bora ya kuigwa kutokana na baadhi ya wataalamu kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kuwa viongozi wa maadili na taaluma katika jamii.

“Zamani vijana wengi walikuwa wakihamasishwa kufikia ndoto zao kwa kuona mifano ya madaktari na wataalamu waliokuwa na maadili na moyo wa kuwahudumia wananchi, lakini hali hiyo imeanza kupungua katika jamii ya sasa,”amesema.

Aidha, amewataka madaktari bingwa kutopimwa kwa idadi ya nyadhifa walizoshika, bali kwa mchango walioutoa katika kuwaokoa wagonjwa, kuwainua wataalamu wengine na kuboresha afya ya jamii kwa ujumla.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha madaktari wa magonjwa ya ndani Tanzania (APHYTA), Dkt. Kajiru Kilonzo amesema wajibu wao kwasasa mpya na wakimkakati ni kuwa viongozi wabunifu na washauri katika kutekeleza mikakati endelevu ya afya nchini.

“Sisi ndio tulio na dhamana ya kutafsiri tafiti za kisayansi kuwa sera zinazoweza kutekelezeka ili kuokoa maisha ya Watanzania kabla hawajafika kwenye vitanda vya mahututi,”amesema.

Mkutano huo pia umesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya utafiti, ukusanyaji wa takwimu na matumizi ya taarifa sahihi katika kufanya maamuzi ya kisera na kupanga huduma bora za afya.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!