Home Kitaifa SHIRIKI TBS ” VIWANGO MARATHON ” MEI , 23 KUCHANGIA VIFAA KWENYE...

SHIRIKI TBS ” VIWANGO MARATHON ” MEI , 23 KUCHANGIA VIFAA KWENYE HOSPITALI ZENYE UHITAJI .

 Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeandaa mbio za marathon zijulikanazo kama ‘Viwango Marathon’ ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa shirika hilo, huku likihamasisha matumizi ya bidhaa zilizothibitishwa na TBS pamoja na kuimarisha afya kwa jamii kupitia michezo.

Marathon hiyo inayotarajiwa kufanyika Mei 23, 2026 katika viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, imebeba ujumbe mpana wa kuhamasisha matumizi ya bidhaa zilizothibitishwa na TBS sambamba na kurejesha kwa jamii kupitia msaada wa vifaa mbalimbali kwa hospitali zenye uhitaji.

Katika kipindi ambacho taasisi nyingi huadhimisha mafanikio yao kwa sherehe na matukio rasmi pekee, TBS imechagua njia yenye kugusa jamii moja kwa moja kwa kuunganisha michezo, afya na huduma kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Afisa Ukaguzi wa TBS, Mhandisi Nyabuchwenza Methusela amesema mbio hizo zimeandaliwa kwa lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali katika kuchangia ustawi wa jamii huku zikitoa nafasi ya kusaidia hospitali zinazokabiliwa na changamoto za vifaa tiba.

Amesema sehemu ya mchango utakaochangiwa kupitia wadhamini na washiriki wa marathon hiyo utaelekezwa katika utoaji wa vifaa muhimu kwa hospitali zenye mahitaji, hatua inayotarajiwa kuongeza matumaini kwa wananchi wanaotegemea huduma hizo.

“Tunataka maadhimisho haya ya miaka 50 yawe na alama kwa jamii. Ndiyo maana kupitia Viwango Marathon tunalenga kuhamasisha afya, matumizi ya bidhaa zenye viwango lakini pia kusaidia hospitali zinazohitaji vifaa mbalimbali,” amesema Mhandisi Nyabuchwenza.

Hatua hiyo imepokelewa kama mfano wa namna taasisi za umma zinavyoweza kutumia matukio ya kijamii kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi, hasa katika sekta ya afya ambayo bado ina mahitaji makubwa ya vifaa na huduma katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa upande wake, Afisa Ukaguzi wa TBS, Mhandisi Hassani Zaidi Amiri amesema marathon hiyo itahusisha mbio za kilometa tano, kilometa 10 pamoja na kilometa 21 ili kutoa nafasi kwa watu wa makundi tofauti kushiriki kulingana na uwezo wao wa kukimbia.

Mbali na ushindani wa michezo, Viwango Marathon inatajwa kuwa jukwaa la kuunganisha wadau wa afya, michezo, biashara na wananchi katika ujumbe mmoja wa kusaidia jamii na kuhamasisha ubora wa bidhaa zinazotumiwa nchini.

Wananchi, taasisi, kampuni binafsi pamoja na wadau wa michezo wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kushiriki marathon hiyo kwa gharama ya shilingi 30,000 kwa kila mshiriki, fedha ambazo pia zitakuwa sehemu ya safari ya kusaidia hospitali zenye uhitaji.

Usajili wa kushiriki marathon hiyo unapatikana kupitia events.tbs.go.tz

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!