
Mbunge wa Jimbo la Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa, ametimiza ahadi ya kutoa shilingi milioni tano kwa ajili ya kufanikisha kambi ya michezo ya UMISETA 2026 katika Wilaya ya Biharamulo.
Fedha hizo zimekabidhiwa kwa niaba yake na Katibu wa Idara ya Siasa na Mawasiliano ya Umma wa ofisi yake, Baraka Mugusi, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa Februari 21, 2026 wakati wa tamasha la ugawaji wa vifaa vya michezo kwa shule 35 za sekondari wilayani humo.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mugusi amesema ofisi ya mbunge itaendelea kushirikiana na sekta ya elimu kuboresha mazingira ya walimu na wanafunzi pamoja na kuhamasisha ushiriki wa michezo ili kuongeza ufaulu mashuleni.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Biharamulo, Ndabazi Stephano, amesema mchango huo utasaidia kufanikisha kambi maalum ya UMISETA inayotarajiwa kufanyika kwa mara ya kwanza wilayani humo.
Amesema uwepo wa kambi hiyo utawawezesha wanafunzi kushiriki michezo katika mazingira bora na kuongeza ari ya ushindani pamoja na maendeleo ya michezo mashuleni.
Makabidhiano hayo yalifanyika mbele ya Kamati Maalum ya Uratibu wa Michezo ya UMISETA 2026 Wilaya ya Biharamulo iliyoongozwa na Asimwe Bora pamoja na wajumbe wengine wa kamati hiyo.









