
Wadau wote wanaohusika na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mfumo huo na kutumia fursa hiyo kujenga ushirikiano utakaosaidia kukuza biashara na uchumi wa Taifa.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala yaliyofanyika jijini Dodoma, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo, “Mfumo Imara, Uchumi Endelevu”.

Naibu Waziri Londo amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, mfumo huo umekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha biashara ya mazao kwa kuongeza matumizi ya maghala yenye viwango, kuboresha uhifadhi na kujenga uaminifu katika soko la mazao nchini.
Amesema maadhimisho hayo yanafanyika wakati muafaka ambapo Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya biashara, kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi na kuweka mazingira bora ya ushindani.

“Kupitia mfumo huu, kumekuwa na ongezeko la ushiriki wa wakulima, vyama vya ushirika, sekta binafsi na taasisi za kifedha katika biashara ya mazao, hali iliyochangia kuimarika kwa mazingira ya biashara na uchumi katika maeneo mbalimbali nchini,” alieleza Naibu Waziri Londo.
Aliongeza kuwa maonesho hayo, pamoja na mijadala iliyoandaliwa, yanalenga kutoa fursa kwa wadau kubadilishana uzoefu, kuonesha huduma na bidhaa zao, na kujadili namna ya kuimarisha mfumo huo ili uendane na mahitaji ya sasa ya kiteknolojia pamoja na ushindani wa masoko ya kikanda na kimataifa.
Aidha, Naibu Waziri Londo alisisitiza kuwa maadhimisho hayo ni kielelezo cha mchango mkubwa wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala katika kuimarisha biashara ya mazao, jambo linalochangia kwa vitendo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.









