Na Mwandishi Wetu.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kudhihirisha nafasi yake muhimu katika maendeleo ya sekta ya Viwanda, Biashara na Ubora wa bidhaa baada ya kushiriki Mkutano wa 28 wa Kamati ya Viwango ya Afrika Mashariki (EASC) uliofanyika katika Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha kuanzia Mei 12 hadi 14, 2026.
Mkutano huo umekutanisha wataalamu wa viwango, ubora wa bidhaa, metrolojia na upimaji kutoka nchi wanachama wa EAC kwa lengo la kujadili na kutekeleza mpango kazi wa Standards, Testing, Metrology and Quality (SQMT), ambao unalenga kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ushiriki wa TBS katika mkutano huo unaendelea kuonyesha dhamira ya Tanzania katika kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya kimataifa, hatua inayosaidia kuongeza ushindani wa bidhaa za Kitanzania katika soko la kikanda na kimataifa.
Kupitia ushiriki huo, TBS imeendelea kuwa nguzo muhimu katika kulinda afya na usalama wa walaji huku ikiwezesha mazingira bora ya biashara na ukuaji wa viwanda vya ndani. Wadau mbalimbali wameendelea kupongeza mchango wa shirika hilo kwa namna linavyoisimamia sekta ya viwango kwa weledi mkubwa na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa sehemu ya maamuzi muhimu yanayohusu ubora wa bidhaa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha, mkutano huo umefungua fursa mpya za ushirikiano wa kitaalamu baina ya nchi wanachama, jambo litakalosaidia kuboresha mifumo ya viwango, kuondoa vikwazo vya biashara na kuongeza ufanisi wa bidhaa zinazovuka mipaka ya nchi za EAC.
Kwa miaka ya hivi karibuni, TBS imeendelea kufanya mageuzi makubwa katika huduma zake kwa kuimarisha maabara za upimaji, kuongeza matumizi ya teknolojia pamoja na kutoa elimu kwa wazalishaji kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango. Hatua hizo zimeifanya Tanzania kuendelea kujijengea heshima katika sekta ya ubora wa bidhaa ndani na nje ya nchi.
Ushiriki wa TBS katika Mkutano wa 28 wa EASC ni ishara ya namna Tanzania ilivyojipanga kuhakikisha bidhaa zake zinaendelea kuwa salama, bora na zenye ushindani mkubwa katika soko la Afrika Mashariki na duniani kwa ujumla.











