
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi amesema Serikali imefanya juhudi mbalimbali za kisera, kisheria na kimkakati ili kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki na Kati.
Dkt. Yonazi aliyasema hayo katika kikao cha Kikundi Kazi cha Mazingira ya Biashara cha Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema Serikali imefanya jitihada za kukuza biashara nchini, huku akizitaka sekta binafsi kuendelea kushirikiana na Serikali.

“Serikali imefanya juhudi mbalimbali katika uwekezaji nchini, ikiwemo kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara kisera na kisheria, kwa lengo la kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha biashara Afrika Mashariki na Kati,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dkt. Godwill Wanga, alisema kikao hicho kimefanyika ili kujadili maendeleo ya biashara nchini.
Alisema kikao hicho kimejadili vivutio ambavyo Serikali inaweza kuviimarisha ili kuongeza uwekezaji zaidi katika sekta ya afya, hasa katika maandalizi ya utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, ili iweze kuwa na manufaa kwa Watanzania.
“Kikao hiki ni muendelezo wa vikao ambavyo tumekuwa tukifanya mara kwa mara kujadili maendeleo ya biashara. Katika kikao hiki, pia tumejadili kuhusu miundombinu ya mtandao katika nchi yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa: “Tumekubaliana kufanya utafiti kuhusu madhara ya vita katika Mashariki ya Kati kwa uchumi wetu.”








