Home Kitaifa 𝗞𝗜𝗣𝗘𝗡𝗚𝗔 𝗖𝗛𝗔𝗣𝗨𝗟𝗜𝗭𝗪𝗔 𝗞𝗨𝗪𝗔𝗦𝗜𝗟𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗠𝗜𝗦𝗪𝗔𝗗𝗔 𝗬𝗔 𝗧𝗨𝗭𝗢 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗜𝗙𝗔 𝗬𝗔 𝗠𝗪𝗔𝗟𝗜𝗠𝗨 𝗡𝗬𝗘𝗥𝗘𝗥𝗘 𝗬𝗔...

𝗞𝗜𝗣𝗘𝗡𝗚𝗔 𝗖𝗛𝗔𝗣𝗨𝗟𝗜𝗭𝗪𝗔 𝗞𝗨𝗪𝗔𝗦𝗜𝗟𝗜𝗦𝗛𝗔 𝗠𝗜𝗦𝗪𝗔𝗗𝗔 𝗬𝗔 𝗧𝗨𝗭𝗢 𝗬𝗔 𝗧𝗔𝗜𝗙𝗔 𝗬𝗔 𝗠𝗪𝗔𝗟𝗜𝗠𝗨 𝗡𝗬𝗘𝗥𝗘𝗥𝗘 𝗬𝗔 𝗨𝗔𝗡𝗗𝗜𝗦𝗛𝗜 𝗕𝗨𝗡𝗜𝗙𝗨

Na.Mwandishi Wetu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesema Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu imeendelea kuonyesha mafanikio makubwa, ambapo tangu kuanzishwa kwake Watanzania 27 wamefanikiwa kushinda katika nyanja mbalimbali za uandishi bunifu.

Amesema mafanikio hayo yanaonyesha namna tuzo hiyo inavyoibua na kutambua vipaji vya waandishi bunifu nchini, huku idadi ya washiriki ikiongezeka kila mwaka kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Prof. Mkenda amebainisha kuwa Serikali imewekeza takribani Shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuchapisha vitabu vilivyoshinda tuzo hizo na kuvisambaza katika shule za Tanzania Bara na Zanzibar, hatua inayolenga kuwafikia wasomaji wengi zaidi na kuhamasisha utamaduni wa kusoma.

Aidha, Waziri Mkenda amesema tuzo hizo zimeendelea kukua na kuvutia washiriki kutoka mataifa mbalimbali, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa hadhi yake na umuhimu wa uandishi bunifu katika kukuza fasihi na lugha ya Kiswahili.

Ameongeza kuwa tuzo hizo zimekuwa jukwaa la kuwahamasisha vijana na waandishi kutumia vipaji vyao katika kutengeneza kazi zenye ubunifu na maudhui yanayoweza kuelimisha na kujenga jamii.

“Tuzo hii sasa imeingizwa rasmi katika orodha ya tuzo za uandishi bunifu duniani, ukiitafuta mtandaoni utaona tarehe 13 Aprili ni siku ya kutoa Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu,” amesema Prof. Mkenda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Prof. Penina Mlama, amesema dirisha la kuwasilisha miswada ya kazi za ubunifu limefunguliwa rasmi leo, Agosti 19, 2026, na litafungwa Novemba 30, mwaka huu.

Ameeleza kuwa waandishi bunifu wanatakiwa kutumia kipindi cha takribani miezi mitatu kuwasilisha miswada yao, huku matangazo yenye vigezo na taratibu za kushiriki yakitolewa kupitia mitandao ya kijamii ya tuzo hiyo pamoja na mitandao ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Elimu Tanzania.

Prof. Mlama amesema mshiriki anatakiwa kuwa raia wa Tanzania, kazi iwe imeandikwa kwa Kiswahili na kila mwandishi anaruhusiwa kuwasilisha andiko moja tu katika nyanja atakayochagua. Aidha, mswada unaowasilishwa unatakiwa kuwa haujawahi kuchapishwa popote.

Amefafanua kuwa miswada iliyowahi kushika nafasi ya kwanza hadi ya 10 katika miaka iliyopita haitaruhusiwa kuwasilishwa tena, ingawa waandishi waliowahi kushika nafasi hizo wanaweza kushiriki kwa kuwasilisha miswada mipya. Pia, miswada iliyowahi kushinda tuzo nyingine haitazingatiwa katika ushindani wa mwaka huu.

Kwa upande wa vigezo mahususi, tamthilia ya jukwaani inapaswa kutumia vionjo vya sanaa za maonyesho za Tanzania, iwe na muda wa dakika 40–60, isiwe na maonyesho zaidi ya sita na wahusika wasiozidi sita. Ushairi unatakiwa kuwa na mashairi yasiyopungua 50 wala kuzidi 60, huku kila shairi likiwa na beti zisizozidi 15.

Kwa riwaya, urefu unatakiwa kuwa kati ya maneno 60,000 na 100,000, wakati hadithi za watoto zinatakiwa kuwa na kati ya maneno 250 na 500 kwa hadithi moja. Prof. Mlama amesisitiza kuwa kazi zinazowasilishwa zinapaswa kuwa na mawazo asilia ya mwandishi na kujikita katika masuala muhimu ya jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!