
Msanii wa Bongo Fleva mwenye sauti ya kipekee, Yammi, sasa anatua rasmi katika hatua mpya ya maisha yake ya muziki baada ya kumaliza mkataba wake na lebo ya The African Princess, inayomilikiwa na Nandy.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa Mei 5, 2025, na uongozi wa The African Princess, imeelezwa kuwa Yammi ameachana na lebo hiyo kwa makubaliano mema, huku akipata wawekezaji wapya wanaomuandalia safari ya kimataifa.
“The African Princess Records inapenda kuwataarifu rasmi wadau wa muziki, vyombo vya habari, na mashabiki wote kuwa msanii wetu mpendwa Yasirun Yasin Shaban, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Yammi, amehitimisha rasmi mkataba wa usimamizi wa kazi zake na lebo yetu kwa makubaliano ya kirafiki na kwa manufaa ya pande zote mbili.“
The African Princess wameeleza kuwa Yammi amekua na kupevuka kisanii kupitia lebo hiyo, na sasa wanajivunia kumuona akichukua hatua mpya akiwa chini ya wawekezaji wapya watakaomsukuma mbele zaidi.








