Na Shomari Binda-Musoma
HALMASHAURI ya Wilaya ya Serengeti imejipanga kuwa na mashamba darasa kila Kata ili wananchi waweze kujifunza nakufanya kilimo cha tija.
Kauli hiyo ilitolewa na kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Bwenda Bainga kwenye kikao cha mwaka cha baraza la madiwani.
Akijibu maswali ya papo kwa papo ya madiwani Bainga ambaye ni afisa kilimo na mifugo wa halmashauri hiyo amesema maafisa kwenye Kata zote 30 wanapaswa kushirikiana na maafisa ugani kuwa na mashamba hayo.
Amesema serikali inalipa mishahara kwa maafisa ugani na watumishi wengine kwenye Kata ili kuweza kuwasaidia wananchi na mashamba darasa ni sehemu ya majukumu yao.
Kaimu mkurugenzi huyo amesema katika msimu wa mvua unaokuja kila Kata zitakuwa na shamba darasa japo moja ili wananchi wajifunze.
“Serikali ya Rsis Dkt.Samia Suluhu Hassan,inataka kilimo nchi hii kiweze kuwanufaisha wananchi hivyo ni muhimu kuwa na mashamba darasa”
“Najua ipo changamoto ya usafiri kuzungukia maeneo yote lakini tutajitahidi walau kuwa na shamba darasa moja kila Kata” amesema Bainga.
Amesema kwa kuwa anasimamia kilimo kwenye halmashauri hiyo amewahakikishia madiwani kusimamia zoezi hilo na kufanikiwa.
Baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo wamesema kuwepo kwa mashamba darasa kutawasaidia wananchi kufanya kilimo ambacho kitainua uchumi wao na kusomesha watoto.








