
Na. Benny Mwaipaja, Zanzibar
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuendelea kuboresha mikakati ya ukusanyaji wa mapato kwa kuimarisha usimamizi wa masuala ya forodha, matumizi ya takwimu sahihi na ushirikiano na wadau wa biashara, ili kuongeza ufanisi wa makusanyo na kusaidia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya Serikali.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika Ofisi za TRA Zanzibar, Mhe. Balozi Omar amesema ziara hiyo imelenga kutathmini mwenendo wa makusanyo, kujadiliana kuhusu changamoto zilizopo na kubaini fursa za kuboresha utendaji katika kipindi kilichosalia cha mwaka wa fedha.
Mhe. Balozi Omar alisema katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, TRA Zanzibar imekusanya shilingi bilioni 216.3 kati ya lengo la shilingi bilioni 245.6, sawa na ufanisi wa asilimia 88 huku kukiwa na nakisi ya makusanyo ya zaidi ya shilingi bilioni 29.

Amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kuimarisha juhudi za ukusanyaji wa mapato, hususan katika Idara ya Forodha, ili kufikia malengo yaliyowekwa nankuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo ya jamii.
“Katika mwenendo wa makusanyo, uchambuzi wa kina wa takwimu ni muhimu katika kubaini mabadiliko ya biashara na sababu zinazochangia kupanda au kushuka kwa mapato na uchambuzi huo unapaswa kuzingatia aina, kiasi na thamani ya bidhaa zinazoingia Zanzibar, pamoja na mabadiliko ya shughuli za kiuchumi na miradi ya maendeleo” alisema Mhe. Balozi Omar.
Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya TRA na Shirika la Bandari Zanzibar -ZPC ni muhimu katika kulinganisha takwimu za mizigo na mwenendo wa mapato, ili kuwezesha Serikali kupata taarifa sahihi na kufanya maamuzi yanayozingatia hali halisi ya biashara.
Aidha, ameitaka Idara ya Forodha kuendelea kuimarisha mifumo ya ukaguzi na uthamini wa bidhaa, pamoja na uhakiki wa nyaraka za uingizaji na uuzaji nje ya nchi, ili kuhakikisha kodi zinazostahili zinakusanywa kwa usahihi na kwa wakati.
Katika kuimarisha ushirikiano na uwajibikaji, Mhe. Balozi Omar alipendekeza kuwepo kwa viashiria vya utendaji kwa washauri wa kodi na mawakala wa uondoshaji mizigo bandarini (Clearing and Forwarding Agents), kwa kuzingatia majukumu yao katika mfumo wa kodi, akisisitiza umuhimu wa kuharakisha utatuzi wa mashauri ya kodi yaliyodumu kwa muda mrefu ili kurahisisha ulipaji wa kodi na kuboresha utoaji wa huduma kwa walipa kodi.

“Serikali inategemea mapato yanayokusanywa kugharamia huduma muhimu kwa wananchi, ikiwemo afya, mishahara na mahitaji mengine ya maendeleo, na kwa msingi huo, nawahimiza TRA kuendelea kutumia takwimu, teknolojia na ushirikiano na wadau katika kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato” alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Bw. Mcha Hassan Mcha, alisema kuwa TRA itaendelea kufanyia kazi maelekezo ya Serikali katika kuboresha ukusanyaji wa kodi ili kusaidia kufikia malengo ya maendeleo ya nchi.
Bw. Mcha alisema kuwa Ofisi ya TRA Zanzibar imewekewa lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.144 ambayo ni sawa na asilimia 34 ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa mujibu wa bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambazo zinatarajiwa kutumika katika shughuli za maendeleo na kwamba watafanya jitihada kuhakikisha kuwa lengo hilo linafikiwa.
MWISHO










