
Na Deborah Lemmubi-Mzawa Media Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph amewaomba wananchi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha wanasaidia kuzilinda mita za maji ikiwemo kuzijengea kiboksi ili zisiweze kuchukuliwa kirahisi.
Kwani hivi karibuni DUWASA imekutana na changamoto ya wizi wa mita hizo baada ya wananchi kulalamika kuibiwa ambapo ndani ya miezi mitatu takwimu zimeonesha kuwa mita 103 zimeibiwa ikiwa ni wastani wa zaidi ya mita 30 kwa mwezi.

Mhandisi Aron ameyasema hayo Jijini Dodoma Oktoba 26,2026 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akitoa Taarifa ya hali ya huduma ya Majisafi na utekelezaji wa miradi na uhujumu wa Miundombinu ya DUWASA.
“Katika vitu ambavyo vinatupa changamoto hapa Jiji la Dodoma ni wizi wa mita,wananchi wengi wanalalamika kuibiwa mita hasa ambao mita zao ziko nje ya uzio, ndani ya miezi mitatu takwimu zinaonesha kwamba mita 103 zimeibiwa ni kama wastani wa mita zaidi ya 30 hivi kwa kila mwezi,ambapo hilo ni jambo la hatari“.

Aidha amesem kuwa mara baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wameweza kufanya uchunguzi ambapo wamegundua wengi wanapoiba mita hizo wanaenda kuyeyusha na kutengeneza bangili,pete na wengine hupeleka kuuza katika mizani ya chuma chakavu.
Mbali na hilo pia amebainisha changamoto iliyopo upande wa miundombinu ya maji taka kuwa ni wizi wa mifuniko ya chemba za majitaka ambazo nazo huuzwa katika chuma chakavu na kuwataka wanunuzi kuwa wazalendo kwa kuacha kununua kwani mifuniko hiyo ina nembo ya DUWASA.
Pamoja na kuwataka wananchi wote kutoa Taarifa DUWASA au katika Jeshi la Polisi mara wanapopata Taarifa sahihi juu ya wizi huo wa mita na mifuniko ya chemba.









