
Na Deborah Lemmubi-Mzawa Media Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Bwana Gerson Msigwa ametoa Wito kwa vijana kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza fursa zitakazo waingizia kipato na si kuitumia kwa kuhamasisha uvunjifu wa sheria.
Msigwa ameyasema hayo leo Jijini Dodoma Oktoba 25,2026 wakati akizungumza na Waandishi wa Habari akielezea mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali pamoja na kutoa taarifa kuhusu Uzinduzi rasmi wa Mji wa Serikali utakaofanyika tarehe 30 Oktoba 2026 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

“Wito wangu, vijana tumieni mitandao kutengeneza pesa, kujifunza, kutafuta masono, kupata burudani, kutengeneza connections za kupata hela na sio kuhamasishana kuvunja sheria. Hakuna aliyefanikiwa kwa kushiriki uhalifu, ukifanya uhalifu unajiharibia future yako“.
Na kuongeza kuwa vijana ndio watumiaji wakubwa wa mitandao ambayo ndio imekuwa ikitumika kuhamasisha vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani,hivyo wanapaswa kuwa makini sana kwani yote yanayoendelea mitandaoni vyombo vya ulinzi na usalama vinayaona, na wote wanaojihusisha na uchochezi huo wanafuatiliwa.

Mbali na Vijana pia ametoa wito kwa Watanzania wote, kuendelea kujiepusha kushiriki katika matukio yoyote yenye viashiria vya vurugu na uvunjifu wa amani.
“Watanzania wakataeni watu wote ambao wanadhani wanaweza kufanikisha ajenda zao kwa kuwahamasisha kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria. Wasikilizeni lakini wapuuzeni kwa sababu pakichafuka hapa hakuna mjomba wa kutusaidia zaidi ya sisi wenyewe. Kubomoa ni rahisi lakini kujenga upya ni mchakato mrefu na mifano ipo mingi”.
“Aidha, naomba kuwahakikishia kuwa Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama vipo imara kuhakikisha vinasimamia amani na usalama wa watu na mali zao pamoja na usalama wa mipaka ya nchi“.
Msigwa ameeleza kuwa mafanikio ya utekelezaji wa Dira 2050 ambayo imewekewa malengo makubwa ya kujenga uchumi wa Dola za Marekani Trilioni 1 ikilinganishwa na uchumi wa sasa ambao ni takribani Dola Bilioni 90, yanahitaji uwajibikaji wa pamoja kwa wadau wote katika Serikali ambayo itachangia uchumi huo kwa asilimia 30 na Sekta Binafsi inayotarajiwa kuchangia katika uchumi huo kwa asilimia 70.
Hivyo ili kufanikiwa inahitaji nchi yenye amani na utulivu ili kuweza kujikita katika uzalishaji, biashara hasa ya nje na kuinua ustawi wa jamii.
Kwani malengo hayo hayatafikiwa kama muda mwingi utapotezwa kuhamasishana kufanya vurugu ama kufanya mambo ambayo yanayokwamisha au kuchelewesha uzalishaji mali, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuimarisha huduma kwa wananchi.









