Home Kitaifa WAZIRI SANGU AZINDUA BODI YA SABA YA USHAURI YA OSHA

WAZIRI SANGU AZINDUA BODI YA SABA YA USHAURI YA OSHA

-Asisitiza Utekelezaji wa Viwango vya Kimataifa vya Usalama na Afya katika Maeneo ya Kazi

Na, OWM-KAM 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Sangu, amezindua Bodi ya Saba ya Ushauri ya Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakala za Serikali, Sura ya 245 Toleo la mwaka 2023 chini ya Kifungu cha 6 cha sheria hiyo.

Amezungumza  hayo tarehe 25 Mei, 2026 wakati wa uzinduzi huo, Waziri Sangu amesema bodi hiyo ina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu kwa OSHA ili kuimarisha utendaji wa taasisi hiyo na kuhakikisha mikakati inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kwa kuzingatia dira, dhima na malengo ya Serikali.

Amesema kuwa miongoni mwa majukumu ya bodi hiyo ni kushauri kuhusu uandaaji na utekelezaji wa mpango mkakati wa OSHA, kufanya tathmini ya utendaji wa taasisi kupitia taarifa za mwaka na hesabu za wakala, pamoja na kutoa ushauri kuhusu maslahi na stahili za watumishi kwa lengo la kuongeza motisha, uwajibikaji na tija mahali pa kazi.

Katika hatua nyingine, Waziri Sangu ameielekeza bodi hiyo kusimamia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 155 na 187 ili kuhakikisha viwango vya kimataifa vya usalama na afya mahali pa kazi vinaendelea kuzingatiwa nchini.

Aidha, ameitaka bodi hiyo kuimarisha mifumo ya utoaji huduma kwa njia ya kidijitali, ikiwemo mfumo wa Workplace Information Management System (WIMS), kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na wadau mbalimbali.

“Majukumu haya yatekelezwe kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni, taratibu na miongozo inayotolewa na Serikali pamoja na misingi ya uwajibikaji, uadilifu, ubunifu, ushirikiano kazini na uwazi” amesema Waziri Sangu.

Sambamba na hilo, amesema bodi hiyo inaanza majukumu yake katika kipindi muhimu ambapo Serikali inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, huku uzinduzi wa Mpango Mkakati wa OSHA ukiwa chachu ya utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo.

Waziri Sangu pia ameisisitiza bodi hiyo kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo iliyowekwa, huku akiitaka kutoa nafasi kwa menejimenti ya OSHA kusimamia shughuli za kila siku bila kuingiliwa. Amesema jukumu kuu la bodi ni kutoa ushauri na usimamizi wa kimkakati ili kuhakikisha kila upande unatekeleza wajibu wake ipasavyo.

Akizungumza Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri OSHA, Makwaia Makani, ameishukuru Serikali kwa imani iliyowaonesha na kuahidi kuwa bodi hiyo itatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyowekwa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bi. Zuhura Yunus, amewapongeza wajumbe wa bodi kwa kuaminiwa na kuteuliwa, akiwataka kutumia weledi na umahiri wao katika kuisimamia OSHA kwa manufaa ya taasisi na taifa kwa ujumla.

Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema bodi zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya taasisi hiyo na kwamba menejimenti ya OSHA ipo tayari kushirikiana na bodi mpya ili kuendelea kuimarisha utendaji na utoaji wa huduma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!