Home Kitaifa WANAWAKE WAONGOZA MABADILIKO YA TAIFA

WANAWAKE WAONGOZA MABADILIKO YA TAIFA

Jukwaa la wanawake viongozi nchini, Women in Leadership Forum (WLF), limejitambulisha rasmi kwa umma likieleza dhamira yake ya kuunganisha wanawake walio katika nafasi za uongozi ili kujenga sauti ya pamoja, kuimarisha mshikamano wa kitaifa, na kuchangia maendeleo ya Tanzania.

Jukwaa hilo linaongozwa na kaulimbiu isemayo “Women Leading Change in the Future,” likilenga kupanua ushawishi wake katika ngazi ya kitaifa, kikanda, na kimataifa.

Akizungumza leo Aprili 24, 2026 jijini Dar es Salaam katika mkutano huo, Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Dkt. Evaline Munisi, amesema taasisi hiyo ilianzishwa Novemba 2025 na kusajiliwa rasmi Januari 14, 2026, chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Amefafanua kuwa WLF si jukwaa la kisiasa, bali ni la kijamii na kiuongozi, linalowaunganisha wanawake kutoka vyama mbalimbali waliowahi kushiriki katika uchaguzi mkuu kwa lengo la kuendeleza umoja wa kitaifa na maendeleo.

Jukwaa hili ni ushahidi kuwa licha ya tofauti za kiitikadi, viongozi wanaweza kushirikiana kwa maslahi mapana ya taifa,” amesema.

Amewataka Watanzania kuendelea kulinda amani, kuheshimu tofauti za maoni, na kuhimiza mazungumzo ya staha.

Amesisitiza kuwa migawanyiko ya kisiasa inaweza kuwa na athari kwa wananchi wa kawaida pamoja na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, Katibu wa jukwaa hilo, Mwajuma Noty, amesema maandalizi ya uzinduzi rasmi yanaendelea, huku tarehe ikitarajiwa kutangazwa hivi karibuni, pamoja na utaratibu wa wanachama kujiunga.

Ameongeza kuwa jukwaa hilo litaendelea kuwaunganisha wanawake kutoka sekta na makundi mbalimbali ili kuimarisha mshikamano, ushirikiano, na mchango wao katika maendeleo ya taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!