Home Kitaifa TGNP YAWAPA WANAWAKE WA VIJIJINI FURSA YA KUJIFUNZA NA KUNUFAIKA NANE NANE

TGNP YAWAPA WANAWAKE WA VIJIJINI FURSA YA KUJIFUNZA NA KUNUFAIKA NANE NANE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Maonesho ya 49 ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, yamekuwa jukwaa muhimu kwa wanawake wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini kujifunza teknolojia mpya za kilimo, kubadilishana mbegu za asili, kutafuta masoko na kujenga sauti ya pamoja katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo.

Wanawake hao wameletwa kwenye maonesho hayo kupitia mradi wa Wanawake wa Vijijini Kuleta Mabadiliko, unaotekelezwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), kwa lengo la kuwawezesha wakulima wadogo kukutana na wadau wa sekta ya kilimo, kujifunza mbinu bora za uzalishaji na kushiriki katika mijadala inayolenga kuimarisha nafasi yao katika maendeleo ya kilimo.

Akizungumza katika maonesho hayoMratibu wa Vituo vya Taarifa na Maarifa kutoka  Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP, Mwajuma Mkombozi, amesema mradi huo unalenga kuwaunganisha wakulima wanawake kutoka maeneo mbalimbali ili wajifunze kutokana na uzoefu wa wenzao, kubadilishana mbegu za asili, kutambua changamoto zinazowakabili na kuziwasilisha kwa pamoja kwa wadau na watunga sera.

Amesema maonesho hayo pia yanawapa nafasi ya kujifunza namna ya kuongeza thamani ya mazao yao, kutafuta masoko mapya na kutambua fursa zinazoweza kuongeza kipato na kuboresha maisha ya familia zao.

Mmoja wa washiriki hao, Stella John kutoka Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, amesema ushiriki wake katika maonesho ya Nane Nane umempa maarifa mapya kuhusu kilimo ikolojia, uongozi wa wanawake na mbinu za kupambana na ukatili wa kijinsia, huku akiahidi kuyapeleka maarifa hayo kwa wanakikundi na jamii yake mara atakaporejea nyumbani.

Kwa upande wake, Martha Charles Mpalu kutoka Gairo mkoani Morogoro amesema maonesho hayo yamewapa fursa ya kuonyesha mbegu walizonazo, kujifunza kutoka kwa wakulima wengine na kujenga mtandao mpana wa ushirikiano utakaowasaidia kuongeza uzalishaji na kupata masoko ya uhakika.

Naye Clara Malle kutoka Mamire mkoani Manyara amesema mafunzo yanayotolewa kupitia mradi huo yameleta mabadiliko makubwa kwa wanawake katika jamii zao, ambapo wengi sasa wameanza kushiriki katika nafasi za uongozi na kufanya maamuzi yaliyokuwa yakitawaliwa na wanaume pekee.

Amesema pamoja na kuhamasisha kilimo ikolojia, wanawake hao wameendelea kuendesha kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia na kuwajengea uwezo wanawake kujitegemea kiuchumi kupitia shughuli za kilimo.

Kwa upande wake, Olpa Major Sekajingo kutoka Wilaya ya Same amesema maarifa aliyopata katika maonesho hayo yatawafikia wakulima wengi kupitia elimu atakayotoa katika kijiji chake. Alisema pia wataendelea kuhamasisha matumizi ya mbegu za asili zinazostahimili ukame na magonjwa, pamoja na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kupinga ukatili wa kijinsia na kujenga mazingira salama kwa watoto wa kike ili waendelee na masomo yao.

Washiriki hao walieleza kuwa ushiriki wao katika Maonesho ya Nane Nane umeongeza uelewa kuhusu kilimo endelevu, biashara ya mazao na uongozi, huku wakitoa pongezi kwa TGNP na mtandao wa PELUM Tanzania kwa kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo na kuwafungulia fursa mpya za maendeleo.

Wamesema kupitia ushirikiano huo, wanawake wa vijijini wanaendelea kujijengea uwezo wa kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo, kuongeza usalama wa chakula na kipato cha familia, huku wakitoa wito kwa wanawake wengine kujitokeza kushiriki katika shughuli za uzalishaji, uongozi na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ili kujenga jamii yenye usawa na maendeleo endelevu.

¨C11C ¨C12C ¨C13C ¨C14C ¨C15C ¨C16C

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!