Home Kitaifa JUKWAA LA MIFUMO YA CHAKULA LAZINDULIWA DAR

JUKWAA LA MIFUMO YA CHAKULA LAZINDULIWA DAR

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

JIJI la Dar es Salaam limezindua Jukwaa la Mifumo ya Chakula litakalokuwa chombo cha kuunganisha wadau mbalimbali katika kuboresha upatikanaji wa chakula salama, bora na chenye lishe kwa wakazi wa jiji hilo.

Uzinduzi wa jukwaa hilo ulifanywa na Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam, John Mrema, ambaye amesema ukuaji wa kasi wa jiji unaongeza mahitaji ya chakula, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mfumo endelevu, jumuishi na unaostahimili changamoto mbalimbali.

Amesema upatikanaji wa chakula jijini unategemea uzalishaji kutoka mikoa mbalimbali nchini, hivyo ni muhimu kuimarisha mifumo ya uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi, usindikaji, masoko na matumizi ya chakula.

Mrema amesema jukwaa hilo litasaidia kuimarisha uratibu na ushirikiano wa wadau, matumizi ya takwimu na ushahidi katika kufanya maamuzi, usalama wa chakula na lishe, pamoja na kuchochea uwekezaji na ubunifu katika sekta ya chakula.

Amesema pia jukwaa hilo litasaidia kujenga mfumo wa chakula wenye uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la watu mijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Rikolto Afrika Mashariki, Kain Mvanda, amesema jukwaa hilo linawakutanisha zaidi ya wadau 80 kwa lengo la kutafuta suluhisho la changamoto zinazohusu upatikanaji na usalama wa chakula.

Mvanda amesema mjadala huo unahusisha mnyororo mzima wa chakula, kuanzia uzalishaji mashambani, usambazaji na uhifadhi hadi matumizi, huku ukilenga kupunguza upotevu wa chakula na kuhakikisha uzalishaji hauharibu mazingira.

Naye Mratibu wa Mradi wa Growing Together, Ronald Mtana, amesema mradi huo unaotekelezwa na Rikolto kwa ufadhili wa NORAD kupitia IDH ulianza mwaka 2024 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2028.

Amesema nchini Tanzania mradi huo unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Morogoro na Mbeya, huku ukifanya kazi na wakulima, sekta binafsi na wajasiriamali wadogo na wa kati.

Mtana amesema katika eneo la majukwaa ya mifumo ya chakula, mradi utashirikiana na Jiji la Dar es Salaam na Dodoma ili kuimarisha ushirikiano wa wadau katika kuboresha mifumo ya chakula mijini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!