Home Kitaifa WAKAGUZI WA NDANI WAASWA KUZINGATIA UADILIFU, WELEDI NA MAADILI KATIKA KULINDA RASILIMALI...

WAKAGUZI WA NDANI WAASWA KUZINGATIA UADILIFU, WELEDI NA MAADILI KATIKA KULINDA RASILIMALI ZA UMMA

Wakaguzi wa ndani nchini wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi, na kwa kuzingatia maadili ya kazi ili kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha fedha za Serikali zinatumika ipasavyo.

Maagizo hayo yalitolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akifungua Mkutano wa Nne wa Wakaguzi wa Ndani ulioandaliwa na Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Nchini (IIA), katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Cate, mkoani Morogoro.

Alisema uadilifu ni nguzo kuu itakayowezesha taasisi za umma kutoa huduma bora na zenye tija kwa wananchi, pamoja na kujenga mfumo imara wa udhibiti utakaosaidia kuziba mianya ya upotevu wa fedha na kuongeza ufanisi katika matumizi ya mali za umma.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imechukua hatua madhubuti kuimarisha uwazi, kujenga imani ya umma, kuzuia rushwa, na kusisitiza uwajibikaji katika matumizi ya fedha. Hivyo, wakaguzi wa ndani wana wajibu wa kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali za umma,” alisema Mhe. Luswetula.

Alisisitiza kuwa thamani ya umma inapatikana pale ambapo hatua za Serikali zinapelekea uboreshaji wa huduma, matumizi bora ya rasilimali, kupungua kwa rushwa na ubadhirifu, pamoja na kuongezeka kwa imani ya wananchi.

“Wakaguzi wa ndani wanachangia thamani hii kwa kuimarisha utawala, usimamizi wa vihatarishi, na mifumo ya udhibiti wa ndani kwa kutoa uhakiki huru na mapendekezo kwa ajili ya maboresho, hali inayowezesha taasisi za umma kufikia malengo yake kwa tija na kwa kuzingatia maadili,” alifafanua Mhe. Luswetula.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya wakaguzi wa ndani na vitengo husika katika kudhibiti rasilimali za umma, kulinda uhuru wa wakaguzi, na kuhakikisha kuwa mapendekezo yanayotolewa baada ya ukaguzi yanafanyiwa kazi kikamilifu.

Vilevile, aliwaasa wakaguzi wa ndani kujiandaa na mabadiliko ya teknolojia kwa kujifunza matumizi ya takwimu, akili bandia, na mifumo ya ukaguzi wa kidijitali ili kurahisisha kazi na kuleta matokeo ya haraka na sahihi.

Mhe. Luswetula alisema ana imani kuwa mkutano wa mwaka huu wenye kaulimbiu, “Kuleta Matokeo kwa Pamoja: Ukaguzi wa Ndani kwa Ajili ya Thamani ya Umma,” utaimarisha mchango wa ukaguzi wa ndani katika sekta ya umma, huku ukiwapa wajumbe wa bodi na menejimenti mbinu za kivitendo za kutekeleza majukumu yao ya usimamizi.

“Kaulimbiu hii inagusa kiini cha utumishi wa umma—kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia uwajibikaji, uwazi, na utawala bora. Inatazama mbele thamani ya ukaguzi wa ndani katika kuleta matokeo chanya pale unapofanya kazi kwa ushirikiano na wadau ili kubadilisha uhakiki, maarifa, na ushauri kuwa matokeo yanayoonekana,” alisisitiza Mhe. Luswetula.

Awali, akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Kenneth Nindie, alisema kuwa kujenga uwezo wa wakaguzi wa ndani ni muhimu katika kuboresha sekta hiyo nchini na kuwawezesha kuendana na mabadiliko ya teknolojia.

Alisema washiriki wa mkutano huo watapata mbinu za kiutendaji na ufahamu wa kina kuhusu namna ya kuboresha ufanisi kazini, huku wakipata fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa wataalamu wengine wa sekta hiyo.

Naye Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Wakaguzi wa Ndani Nchini (IIA), Jonathan Ngoma, alisema mkutano huo umelenga kuwaleta pamoja wadau mbalimbali kujadili masuala ya uongozi bora na namna ya kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa ndani nchini.

Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa Serikali, wajumbe wa menejimenti, wakaguzi wa ndani, wahasibu, wataalamu wa fedha, na wadau mbalimbali muhimu ili kutafakari, kujifunza, na kushauriana jinsi ya kuendelea kuimarisha utawala bora, uwajibikaji, na uwazi katika sekta ya umma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!