
Na Boniface Gideon, TANGA
Jumuiya ya Vijana wa chama cha Mapinduzi ‘UVCCM’ Wilaya ya Muheza,imetoa msaada wa vifaa mbalimbali na vyakula kwa Wanafunzi wenye ulemavu hususani wa Viungo vya mwili na wenye ulemavu wa ngozi ‘Albino’ , wanaosoma katika Shule ya Sekondari Mlingano ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama hicho,Vifaa hivyo ikiwemo madaftari, kalamu, sabuni, mafuta ya kupaka pamoja na bidhaa za vyakula .
Akikabidhi msaada huo, kwaniaba ya Jumuiya hiyo wilaya ya Muheza, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya hiyo, Aziza Mshakangoto , alisema msaada huo ni sehemu ya shukrani kwa Jamii kwakukiamini chama hicho kuendelea kushika dola,

“Kwaniaba ya Jumuiya ya Vijana Wilaya ya Muheza,wakiwemo Madiwani na Mbunge wetu Mwana ‘Fa’, leo tunawakabidhi msaada huu,tunaamini kuwa utakwenda kuwasaidia watu kwa sehemu ya mahitaji yenu, msaada huu ni mdogo lakini inawezekana ikawa ndio ufunguo kwa wengine kuja kutoa msaada mahali hapa, hivyo nitumie fursa hii kuwaomba wadau wengine waje hapa watoe msaada,mana bado mahitaji ni mengi hususani kwa ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi ‘Albino’,na sisi tunaahidi kurudi tena mahali hapa panapo majaariwa ya Mungu” Alisisitiza Aziza
Kwa upande wake ,Diwani wa kata ya Mlingano ,Mujaheed Mukadam , aliishukuru jumuiya hiyo ya Vijana kwa msaada huo ,
“Kwaniaba ya Wananchi wa kata yetu, tunawashukuru sana kwakuja kutusaidia , msaada huu utakwenda kutusaidia kwenye mahitaji muhimu ya Watoto wetu hususani hawa wenye ulemavu,tunawaomba msituchoke hasa pale tunapowasumbua kuwaomba mtusaidie , tunawaomba msiache kuja tena kutusaidia”Alisema Mukadam
Wakati huo huo, Diwani huyo alikabidhi msaada wa vifaa mbalimbali Shuleni hapo ikiwemo jokofu ‘Freezer’ kwa Wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kwaajili ya kuhifadhia vifaa vinavyotumika kutunza ngozi pamoja na pampu ya kuvuta maji ya kisima,
“Naomba nichukue fursa hii kukabidhi msaada huu,waliniomba waliponialika kwenye mahafali mwaka jana,naamini vitakwenda kusaidia sehemu ya mahitaji muhimu ,niwaombe wadau mbalimbali hususani mashirika ,waje watusaidie ,bado tunahitaji misaada zaidi ya hii” alibainisha Diwani Mukadam








