
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua rasmi awamu ya pili ya mashindano ya kupokea mawazo bunifu kutoka kwa umma, hatua inayolenga kupanua wigo wa kodi na kuboresha huduma za kikodi nchini. Kupitia awamu hii, zaidi ya washindi 1,020 wanatarajiwa kujinyakulia zawadi mbalimbali za fedha taslimu, huku mshindi wa jumla akiondoka na kitita cha Shilingi milioni 50.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam Aprili 29, 2026, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, alisema mashindano hayo ni jukwaa muhimu la kuwapa Watanzania nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika mageuzi ya mfumo wa kodi kwa kuwasilisha mawazo yao ya ubunifu.

Alieleza kuwa lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kuwa maboresho yanayofanywa na TRA yanatokana na uhalisia wa wananchi wenyewe, hususan katika maeneo ya kuwezesha biashara, kuongeza ufanisi wa ukusanyaji kodi, na kuimarisha uchumi wa nchi kuelekea kujitegemea zaidi.
Aidha, alisema mawazo yatakayowasilishwa yanatarajiwa kuchangia utekelezaji wa mapendekezo 284 ya Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, ambapo baadhi yake tayari yameanza kufanyiwa kazi, hivyo kuifanya awamu hii kuwa sehemu ya utekelezaji wa mageuzi makubwa ya mfumo wa kodi nchini.
Bw. Mwenda alisisitiza kuwa TRA ni chombo cha wananchi kinachokusanya kodi kwa manufaa ya wananchi, hivyo ni muhimu kuwashirikisha kikamilifu katika kutoa suluhisho la changamoto zilizopo. Aliongeza kuwa mafanikio ya awamu ya kwanza, iliyowezesha wabunifu 9 kung’ara kati ya washiriki 5,681, yamechochea ari ya kuiboresha zaidi awamu ya pili.
Katika kuhakikisha uwazi na ufanisi, alisema TRA imeunda kamati huru itakayoratibu na kuchambua mawazo yote yatakayowasilishwa bila kuhusisha watumishi wa TRA, hatua inayolenga kuongeza imani kwa washiriki. Pia, zawadi zimeboreshwa ili kuvutia ushiriki mpana zaidi kutoka kwa wananchi.
Kwa upande wa maeneo ya kipaumbele, alitaja upanuzi wa wigo wa kodi katika sekta isiyo rasmi, urahisishaji wa mifumo ya ukadiriaji na ulipaji kodi kwa wafanyabiashara wadogo, maboresho ya huduma za kidijitali, pamoja na matumizi ya teknolojia katika utatuzi wa migogoro ya kikodi.
Awali, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Mcha Hassan Mcha, alisema mashindano hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa mfumo wa kodi kwa kuibua suluhisho bunifu zinazotokana na wananchi wenyewe, huku wadau mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa TCCIA, Bw. Boniface Ndengo, wakiipongeza TRA kwa kuimarisha ushirikishwaji wa sekta binafsi na wananchi katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Mipango wa TRA, Dkt. Ephraim Mdee, alisema maboresho yaliyofanyika katika awamu hii yanahusisha vigezo vya ushindani pamoja na muundo wa zawadi, yakilenga kuongeza ubora wa mawazo yatakayopatikana. Alibainisha kuwa uzoefu wa awamu ya kwanza pamoja na maoni ya wadau mbalimbali umewezesha TRA kubuni mfumo imara zaidi utakaohakikisha mawazo bora yanachaguliwa na kuendelezwa kwa manufaa ya taifa.






