Home Kitaifa TIC YAWAKUTANISHA WADAU WA MIRADI YA UWEKEZAJI

TIC YAWAKUTANISHA WADAU WA MIRADI YA UWEKEZAJI

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimewakutanisha wawekezaji na wadau mbalimbali katika kikao kilichofanyika jijini Dar wa Salaam ili kujadili kwa pamoja changamoto za wawekezaji hao na kuzipatia suluhisho ndani ya muda mfupi.

Mnamo mwezi Machi 2023 Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Uwekezaji) Dkt. Tausi Mbaga Kida na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa nyakati tofauti walifanya ziara katika miradi ya kimkakati kwa lengo la kufahamu hatua iliyofikiwa pamoja na changamoto.

Miradi iliyotembelewa ni Kairuki Pharmaceuticals Industries Ltd (Zegereni Kibaha), Sino Tan Kibaha Industrial Park Limited (Kwala Kibaha), Kamaka Co. Lid (Kikongo Kibaha), Elsewedy Electric East Africa Limited (Kisarawe II Kigamboni), Bagamoyo Sugar Limited (Bagamoyo), Goodwill (Tanzania) Ceramic Company Limited (Mkuranga) na Saphire Float Glass (Tanzania) Co. Ltd (Mkuranga).

Kupitia ziara hizo, wajumbe walijionea juhudi kubwa zilizofanywa na wawekezaji katika kutekeleza miradi husika. Lakini pamoja na juhudi kubwa zilizofanywa na wawekezaji husika, miradi inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama ukosefu wa gesi kwenye maeneo ya miradi, kuchelewa kuanza kufanya kazi kwa Bandari kavu ya Kwala, kutokuwa na umeme unaokidhi majitaji ya wawekezaji, uhaba wa maji pamoja na ukosefu wa mifumo ya maji taka.

Akizungumza baada ya kikao hicho Bw. Revocatus Rasheli, Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji kwa Wawekezaji (TIC) amesema wawekezaji wameeleza vizuri baadhi ya changamoto, hali ya utekelezaji na faida za miradi yao nchini.

Taasisi za Serikali za miundombinu zimeweza kuwasiliana na wawekezaji hao hapa na kuwaeleza mipango ambayo wanayo katika kuhakikisha miundo mbinu hiyo inakamilishwa na changamoto hizo zinaondolewa kwa wakati” amesema Bw. Rasheli.

Ameongeza kuwa kwa kiasi kikubwa wadau hao wameonesha kuwa kazi kubwa imefanywa na serikali kwa upande wa miradi ya maji, umeme, barabara na hata miundombinu ya nishatiwya gesi.

Bw. Rasheli amewahakikishia wawekezaji wote wa nje na ndani ya nchi kwamba watakapowekeza Tanzania, Serikali ipo tayari kuhakikisha kwamba changamoto ambazo zinakuwepo zitatatuliwa kabla ya miradi hiyo kuanza kufanya kazi.

Kwa upande wake Mhandisi Felix Nlalio, Katibu Tawala Msaidizi Miundo Mbinu kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani amesema, Mkoa unahakikisha miundombinu yote inafikishwa katika maeneo ya uwekezaji.

Tumekuwa na kamati ya Kitaifa ambayo inasukuma mbele mradi wa kupanga mji wa Kwala ili uweze kuwa na viwanda na biashara hivyo miundombinu yote ni muhimu “ amesema Mhandisi Nlalio.

Nae Bw. Nelson Mollel, Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Kamaka amesema, wamepata majibu mazuri ya changamoto zao tatu za maji, umeme na barabara.

Tumepata uvumbuzi zaidi katika kikao hiki, tumepata uhakika wa kuletewa umeme maana TANESCO wamesema wapo tayari, DAWASA wapo tayari mchakato wa kununua vifaa mzabuni ameshapatikana na barabara ya kutoka Mlandizi kwenda eneo la kongano ya viwanda karibu inaanza kujengwa kwa kiwango cha lami” amemalizia Bw. Mollel.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!