Home Kitaifa TET KUSHIRIKIANA NA DUCE KUIMARISHA ELIMU KUPITIA TAFITI

TET KUSHIRIKIANA NA DUCE KUIMARISHA ELIMU KUPITIA TAFITI

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amefungua maonesho ya Wiki ya Utafiti na Ubunifu ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), huku akiahidi kushirikiana na chuo hicho katika kutumia matokeo ya tafiti kuimarisha ufundishaji nchini.

Akizungumza leo Mei 19, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo yaliyofanyika DUCE, Dkt. Komba amesema tafiti zinazolenga kuboresha ufundishaji, ujifunzaji na mitaala zinapaswa kuwasilishwa TET ili ziweze kufanyiwa kazi na kutumika katika kuboresha sekta ya elimu.

Amesema taasisi hiyo ina jukumu la kuhakikisha wanafunzi kuanzia elimu ya awali wanajengewa misingi imara itakayowawezesha kuwa watafiti na wabunifu mahiri katika siku zijazo.

“Nawapongeza DUCE kwa kutenga wiki hii maalumu kwa ajili ya shughuli za utafiti na ubunifu. Naomba mtumie maarifa haya kuibua hoja zenye manufaa mapana kwa jamii,” amesema Dkt. Komba.

Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE), Profesa Amani Lusekelo Mwamakombe, amesema wiki hiyo inatoa fursa kwa wanataaluma na wanafunzi kuonesha matokeo ya tafiti na bunifu zao pamoja na mchango wake katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.

Profesa Mwamakombe amesema maonesho ya mwaka huu ni ya 11 na yanajumuisha miradi 45. Baadhi ya miradi hiyo imebuniwa na wanataaluma kwa kushirikiana na wanafunzi wao kwa lengo la kutatua matatizo mbalimbali kupitia bidhaa na mbinu bunifu.

Ameeleza kuwa baadhi ya miradi hiyo ipo katika sekta ya elimu, ambapo wataalamu wamebuni mbinu bora za utoaji wa elimu nchini, ikiwemo njia rafiki za kufundisha watoto wa shule za awali.

Aidha, amesema miradi mingine imejikita katika kuboresha namna ya kuwafundisha walimu wa shahada ya kwanza kwa kutumia mbinu rafiki za ufundishaji.

Profesa Mwamakombe ameongeza kuwa tafiti hizo zimechangia kuboresha matokeo ya wanafunzi katika shule mbalimbali nchini kupitia utengenezaji wa vifaa vya kufundishia masomo ya sayansi, ikiwemo hisabati, hatua ambayo imeendelea kuleta tija kwa taifa.

Naye Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa DUCE, Profesa Florence Kyaruzi, amesema moja ya majukumu makuu ya chuo ni kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi kwa jamii, huku akisisitiza kuwa tafiti zao zimejikita katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Profesa Kyaruzi amesema Wiki ya Utafiti na Ubunifu inatoa nafasi kwa chuo kurejesha kwa jamii matokeo ya kazi wanazozifanya pamoja na kuwapa wananchi fursa ya kuwasilisha changamoto mbalimbali ili ziweze kufanyiwa tafiti.

“Hizi kazi tunazifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwemo Global Link. Ushirikiano huo utasaidia kuunganisha nguvu katika kutatua changamoto za jamii na kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Profesa Kyaruzi.

Maadhimisho ya Wiki ya 11 ya Utafiti na Ubunifu yanafanyika kwa siku tatu katika chuo cha DUCE, ambapo wadau mbalimbali wanapata fursa ya kuona tafiti na bunifu zinazotekelezwa na chuo hicho na namna zilivyoleta manufaa kwa jamii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!