
Kaimu Meneja wa usajili wa bidhaa TBS Bi.Noor Meghji akizungumza na waandishi wa habari Kuhusu hatua za kufuata ili kusajili bidhaa za Vipodozi leo Aprili 12,2024 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.

Afisa Viwango (TBS) Bw.Alexander Mashalla akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12,2024 katika Ofisi za TBS Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu.
WAFANYABIASHARA wa bidhaa za Vipodozi nchini wametakiwa kufanya maombi ya usajili wa bidhaa hizo kabla ya kuziingiza katika soko la ndani kutoka nje ya nchi kwa lengo la kulinda usalama kwa watumiaji wa bidhaa hizo.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es Salaam leo Aprili 12,2024 na Kaimu Meneja wa usajili wa bidhaa TBS Bi.Noor Meghji alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwa lengo la kutoa elimu kwa Umma kuhusu taratibu za uingizaji bidhaa za vipodozi sokoni.
Bi.Meghji amesema bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kawaida hupatiwa cheti kinachoidhinisha ubora wa bidhaa hiyo kutoka Shirika la Viwango,ambapo kwa mfanyabiashara anayetaka kuagiza bidhaa za vipodozi,anatakiwa kuomba usajili wa bidhaa hiyo kupitia mfumo unaopatikana kwenye tovuti ya TBS ili zikaguliwe na kujiridhisha ubora wake kabla ya kuingia sokoni.
Aidha Bi.Meghji ameeleza kuwa atakayesajili bidhaa hizo za kutoka nje,kwa mujibu wa Sheria anatakiwa pia kusajili jengo ambalo linatumika kuzihifadhi ambapo itasaidia kurahisisha utunzaji wake ili kuhakikisha usalama kwa watumiaji.








