Home Kitaifa TARURA YATAKIWA KUTEKELEZA MIUNDOMBINU YA BARABARA KABLA YA MSIMU WA MVUA KUANZA...

TARURA YATAKIWA KUTEKELEZA MIUNDOMBINU YA BARABARA KABLA YA MSIMU WA MVUA KUANZA GEITA DC

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Geita umetakiwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara zenye changamoto kabla ya msimu wa mvua kuanza, pamoja na ujenzi wa madaraja ili kurahisisha shughuli za maendeleo.

Hayo yalijiri Novemba 14, 2024, wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani, robo ya kwanza, siku ya pili katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri – Nzera. Katika kikao hicho, baraza lilipokea taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ngazi ya Halmashauri kwa kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2024. Taarifa hizo zilihusu kamati tano za kudumu za Halmashauri ambazo ni: Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango; Kamati ya Uchumi, Ujenzi na Mazingira; Kamati ya Elimu, Afya na Maji; Kamati ya Kudhibiti UKIMWI; na Kamati ya Maadili.

Aidha, kwa mujibu wa kanuni Na. 22 ya kanuni za Halmashauri, madiwani waliuliza maswali ya papo kwa papo na kupatiwa majibu. Katika kikao hicho, madiwani waliiomba ofisi ya TARURA Wilaya ya Geita kuharakisha ujenzi wa barabara zenye changamoto kabla ya msimu wa mvua ili kuepusha madhara yanayoweza kusababishwa na ubovu wa miundombinu.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhandisi kutoka ofisi ya TARURA, Jerry Mwakapemba, alieleza kuwa ofisi ya TARURA inaendelea kutekeleza ujenzi wa miundombinu ya barabara kulingana na bajeti ya kila mwaka. TARURA inahudumia mtandao wa barabara za vijijini (collector feeder and community roads) wenye jumla ya kilometa 1,745.79, zikiwemo barabara za lami (km 4.2), changarawe (km 655.07), na udongo (km 1,086.52), pamoja na madaraja 518.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Mhe. Charles Kazungu, aliitaka TARURA kuongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ili barabara hizo ziweze kutoa huduma kwa wananchi na kuepusha madhara yanayoweza kutokea kutokana na ubovu wa barabara. Kazungu aliongeza kuwa Halmashauri kupitia bajeti zake itatenga kiasi cha fedha kwa ajili ya kuiongezea nguvu TARURA ili kuendelea kukarabati miundombinu ya barabara, kurahisisha shughuli za maendeleo.

Jumla ya shilingi bilioni 1.85 kutoka mfuko wa barabara (Road Fund) imetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara katika majimbo ya Geita na Busanda, shilingi bilioni 1 kutoka mfuko wa majimbo, na tozo ya mafuta kiasi cha shilingi bilioni 2.5.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!