
DAR ES SALAAM
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limeendelea kuthibitisha ubora wake barani Afrika baada ya kutwaa tuzo mbili muhimu katika Tuzo za Kampuni Bora za Mwaka Afrika (Africa Company of the Year Awards – ACOYA).
Katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo iliyofanyika Juni 12, 2026 katika Ukumbi wa Superdome, Oysterbay jijini Dar es Salaam, STAMICO iliibuka mshindi mkubwa wa usiku huo kwa kujinyakulia tuzo ya Shirika Bora la Madini la Mwaka Tanzania pamoja na Tuzo Kuu ya Mshindi wa Jumla wa ACOYA, ambayo ndiyo tuzo kubwa zaidi ya hafla hiyo.
Tuzo hizo zilipokelewa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse, na Meneja wa Masoko na Uhusiano wa Umma wa shirika hilo, Deus Alex Ntukamazina.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kupokea tuzo hizo, Ntukamazina alisema ushindi huo ni wa pili mfululizo kwa STAMICO katika tuzo hizo za bara la Afrika, jambo linaloonesha mafanikio makubwa ya mabadiliko yanayoendelea ndani ya shirika hilo.
Alisema tuzo hizo ni uthibitisho wa kutambuliwa kwa juhudi, ubunifu na kujitolea kwa watendaji wa STAMICO katika kuligeuza shirika hilo kuwa miongoni mwa taasisi zenye ufanisi na kuaminika zaidi katika sekta ya madini.
“Kwa shirika letu, huu ni ushahidi kwamba kazi kubwa inayofanyika katika kulibadilisha STAMICO inatambuliwa na kuthaminiwa. Ni matokeo ya juhudi za pamoja za kuhakikisha tunatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya madini nchini,” alisema Ntukamazina.
Alipoulizwa kuhusu siri ya mafanikio ya STAMICO kutoka kuwa shirika lililokuwa likikabiliwa na changamoto miaka iliyopita hadi kuwa taasisi inayoshinda tuzo za kimataifa, Ntukamazina alieleza kuwa uongozi bora na mipango ya kimkakati ndiyo msingi wa mafanikio hayo.
Alimpongeza Dkt. Mwasse kwa uongozi wake thabiti, bunifu na wenye maono ambao umewezesha STAMICO kupanua shughuli zake za kibiashara, kuongeza gawio kwa Serikali na kuimarisha ushirikiano na wachimbaji wadogo pamoja na wawekezaji wakubwa katika sekta ya madini.
Kwa ushindi huo wa tuzo mbili za bara la Afrika, STAMICO imeendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania na kuweka viwango vya juu vya utendaji kwa mashirika ya umma barani Afrika.









