
Tanzania imefanikiwa kufanya utafiti wa kina wa madini kwa asilimia 16 pekee, huku ikiendelea kutafuta ushirikiano wa kimataifa ili kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti na kupanua wigo wa maarifa kuhusu rasilimali za madini nchini.
Akishiriki ziara rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Urusi tarehe 5 Juni 2026 jijini Moscow, Waziri wa Madini, Mhe. Antony Mavunde (Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Serikali ya Urusi kwenye sekta ya madini ukiongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili (Madini) na Mazingira wa Shirikisho la Urusi, Mhe. Tetenkin Dmitry Dmitrievich.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mavunde alieleza namna sekta ya madini inavyozidi kukua na kuonesha fursa mbalimbali zilizopo kwa wawekezaji nchini, ikiwemo katika eneo la utafiti wa kina.
Mavunde alisema kuwa pamoja na ukuaji wa sekta ya madini, bado kuna haja ya kuongeza eneo linalofanyiwa utafiti wa kina ili kubaini rasilimali zaidi na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya taifa.
Aidha, alimueleza Mhe. Tetenkin kuhusu uwepo wa Hati ya Makubaliano (MoU) baina ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) na chuo kikuu cha Urusi ambayo bado haijakamilika, na kuomba juhudi zaidi ili ikamilike na kuanza kutekelezwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Tetenkin aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kushirikiana na Urusi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kueleza utayari wa nchi yake kuimarisha ushirikiano huo.
Alisisitiza kuwa Urusi ipo tayari kuisaidia Tanzania katika utafiti wa kijiolojia, kuwajengea uwezo wataalamu wa Tanzania na kuandaa MoU ya serikali kwa serikali kupitia Wizara ya Madini ili kuainisha malengo ya pamoja.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alifanya mazungumzo na Bw. Sergey Chestnoy, Mkurugenzi wa Idara ya Kimataifa wa kampuni ya Rusal, na kuialika kampuni hiyo kuja Tanzania kujadili uwekezaji katika utafiti wa kina na uchimbaji wa madini ya bauxite.









