Home Kitaifa SERIKALI YAONGEZA UWEKEZAJI WA BILIONI 52.27 KUIMARISHA ELIMU YA UFUNDI

SERIKALI YAONGEZA UWEKEZAJI WA BILIONI 52.27 KUIMARISHA ELIMU YA UFUNDI

Serikali itaendelea kuongeza uwekezaji mkubwa katika elimu ya ufundi kwa lengo la kuinua ujuzi, ubunifu na uwezo wa ushindani wa vijana katika soko la ajira la ndani na kimataifa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, Desemba 15, 2025 jijini Mwanza wakati wa Mahafali ya 19 ya Duru ya Pili ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza, ambapo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kupitia mradi wa EASTRIP imewekeza Dola za Marekani milioni 16.25 sawa na TZS bilioni 37 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kufundishia teknolojia ya ngozi.

Ameeleza kuwa kupitia mradi wa TELMS II, kiasi cha Euro milioni 5.33 sawa na TZS bilioni 15.27 kimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuboresha ubora wa mafunzo yanayotolewa katika vyuo vya ufundi.

Katika kuimarisha upatikanaji wa elimu ya ufundi nchini, amesema Serikali imeongeza idadi ya wanafunzi walioandikishwa kutoka 161,750 mwaka wa masomo 2023/2024 hadi 199,118 mwaka 2024/2025, huku idadi ya vyuo ikiongezeka kutoka 441 hadi 512.

Amebainisha kuwa Serikali imewajengea uwezo wakufunzi 912 katika ufundishaji wa mitaala ya umahiri, pamoja na kuwapatia mafunzo wakufunzi 45 kuhusu teknolojia mpya katika mnyororo wa thamani wa sekta ya ngozi ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, amesema Serikali imepanga kutoa ithibati kwa vyuo 70 zaidi ili kufikisha jumla ya vyuo 582 vya elimu ya ufundi na ufundi stadi, sambamba na kutoa mafunzo kwa walimu 1,000 na kuhuisha tathmini ya mitaala ya umahiri.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema Serikali imejipanga kuendelea kuwekeza kwa vijana kupitia elimu, hususan elimu ya ufundi na teknolojia, kama mkakati wa kujenga rasilimali watu yenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika maendeleo ya viwanda, uchumi wa kidijitali na matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!