
Serikali ya Awamu ya Sita imeahidi kuendelea kutekeleza ajenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kupitia mkakati wa kuanzisha Kongani za Viwanda na uwekaji wa mazingira wezeshi ya uwekezaji ambapo hadi sasa jumla ya Kongani 34 zimesajiliwa rasmi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaji na Mipango Prof. Kitila Mkumbo (Mb.) akiwa ameambatana na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb.), Waziri wa Maji Mhe. Juma Aweso (Mb.), Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Alhaj Abubakari Kunenge wakati walipotembelea Kongani ya Viwanda ya Kwala iliyopo mkoani Pwani Disemba 10, 2025 kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi wa kongani hiyo na kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili kongani hiyo.

Akibainisha changamoto zilizotatuliwa ni pamoja na changamoto ya umeme wa uhakika, maji ya kutosha, taratibu za usajili wa makampuni, uzalishaji wa bidhaa na uhitaji wa kituo cha reli ya kisasa ya SGR ili kurahisisha usafirishaji wa malighafi na bidhaa zinazotengenezwa kiwandani hapo.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga akizungumza katika kikao hicho amewaahidi wawekezaji hao kuwa wizara yake itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji pamoja na sekta binafsi ikiwemo wawekezaji hao katika kutatua changamoto hizo hususani usajili wa makampuni na upatikaji wa viwango vya ubora vinavyohitajika kwa haraka ili kuendeleza sekta ya viwanda na kuongeza mauzo ya nje.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kongani ya Viwanda ya Kwala Bw. Janson Huang amesema mpaka sasa serikali imewapa wawekezaji ushirikiano wa kutosha katika jitihada za kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa hali inayoendelea kuvutia uwekezaji katika kongani hiyo ambapo hadi sasa viwanda 20 kati ya 200 vimeanzishwa vikitoa ajira 1000 kati ya ajira 100000 zinazotarajiwa kongani hiyo ikikamilika.
Bw. Huang amebainisha miongoni mwa viwanda vilivyoanzishwa ni pamoja na kiwanda cha kutengeneza vifaa vya umeme jua, nguo, friji na kiwanda cha uzalishaji chuma kinatarajia kuanzishwa hivi karibuni.








