
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umemtambulisha rasmi mtoa huduma, kampuni ya Envotec Services Limited, kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Said Mtanda, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku kwa wananchi wa mkoa huo.
Utambulisho huo ni sehemu ya juhudi za Serikali kupitia REA za kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini kwa lengo la kuboresha afya za wananchi, kupunguza matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira pamoja na kuhifadhi mazingira.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mtanda, ameipongeza REA kwa kuendelea kutekeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya nishati yenye manufaa kwa wananchi, ikiwemo mradi wa usambazaji na uuzaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku.
Amesema mradi huo ni muhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwani utasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia, kupunguza matumizi makubwa ya kuni na mkaa pamoja na kusaidia kulinda afya za wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na moshi wa kupikia.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kujitokeza kwa wingi kununua majiko hayo ya ruzuku ili waweze kunufaika na fursa iliyotolewa na Serikali. Amesema matumizi ya majiko banifu yana mchango mkubwa katika kuboresha afya za wananchi, lakini pia katika utunzaji wa mazingira.
“Mkoa wa Mwanza tumeupokea mradi huu kwa mikono miwili kutokana na umuhimu wake kwa wananchi wetu, hususan waishio maeneo ya vijijini na wenye kipato cha chini. Tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mtoa huduma ili kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ubora na unawafikia wananchi walengwa,” amesema Mheshimiwa Mtanda.
Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi kutoka REA, Deusdedith Malulu, ambaye aliambatana na mtoa huduma huyo, amesema jumla ya majiko banifu 9,236 yanatarajiwa kusambazwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza kupitia mradi huo wa ruzuku.
Amesema kwa bei ya kawaida ya dukani, mwananchi angehitajika kulipa kiasi cha Shilingi 50,000 ili kupata jiko hilo, lakini Serikali kupitia mpango huo imetoa ruzuku ya asilimia 85 kwa kila jiko, hali itakayomwezesha mwananchi kununua jiko hilo kwa Shilingi 7,500 pekee.
Mhandisi Malulu ameeleza kuwa wananchi watakaonufaika na mpango huo watapaswa kuwasilisha Kitambulisho cha Taifa (NIDA) wakati wa ununuzi wa jiko hilo ili kuhakikisha ruzuku hiyo inawanufaisha walengwa waliokusudiwa.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Envotec Services Limited, Salma Soud, amesema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa jamii kutokana na manufaa yatokanayo na matumizi ya majiko hayo banifu.
Amesema majiko hayo ni nafuu kwa wananchi na yanasaidia kutunza mazingira kwa kuwa hayatoi moshi mwingi wakati wa matumizi. Pia ameeleza kuwa majiko hayo hutumia kiwango kidogo cha kuni na mkaa, jambo linalosaidia kupunguza gharama za matumizi ya nishati kwa wananchi pamoja na kupunguza ukataji wa miti ovyo.
Bi. Salma ameongeza kuwa kampuni hiyo ipo tayari kushirikiana na Serikali pamoja na wananchi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa mafanikio makubwa na kuwafikia wananchi wengi zaidi katika Mkoa wa Mwanza.
Mwisho.








