Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekamilisha na kuzindua mradi wa kimkakati wa Kituo cha Kubadilishia Njia za Usambazaji Umeme (Switching Station) pamoja na Transforma ya Kudhibiti Umeme katika eneo la Mbande, Wilaya ya Kongwa, uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 10.5.
Mradi huo unahusisha ujenzi wa kituo cha kubadilishia njia za usambazaji umeme, usimikaji wa Transforma ya Kudhibiti Umeme yenye uwezo wa MVA 20 pamoja na ujenzi wa njia mpya ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 92 kutoka Zuzu hadi Mbande.
Akizungumza June 16,2026 Wilayani Kongwa wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema uwekezaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, salama na wenye ubora kwa wananchi na wawekezaji.
Amesema mradi huo umeondoa utegemezi wa njia moja ya umeme iliyokuwa ikitoka Dodoma Mjini kwenda Kongwa, hali iliyokuwa ikisababisha changamoto za kukatika kwa umeme wakati wa matengenezo au hitilafu za kiufundi.
“Mradi huu utaimarisha uthabiti wa mfumo wa usambazaji wa umeme katika Wilaya za Kongwa, Gairo, Chamwino na baadhi ya maeneo ya Mpwapwa,tutaongeza uwezo wa TANESCO kuhudumia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya umeme kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii,” amesema Ndejembi.
Amebainisha kuwa Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati ambapo kwa sasa Tanzania ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya megawati 4,000 za umeme, huku ikilenga kufikia zaidi ya megawati 8,000 katika miaka ijayo ili kuendana na mahitaji ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema kukamilika kwa miundombinu hiyo kutasaidia kupunguza athari za hitilafu kwenye mfumo wa usambazaji wa umeme, kuboresha viwango vya umeme na kuongeza uhakika wa huduma kwa wananchi na wawekezaji.
Ameeleza kuwa uwekezaji huo utafungua fursa mpya za uwekezaji wa viwanda, biashara, kilimo cha umwagiliaji na huduma za kijamii zinazotegemea umeme wa uhakika katika ukanda wa kati wa Tanzania.
“Mkoa wa Dodoma unaendelea kukua kwa kasi kutokana na kuwa Makao Makuu ya Nchi. Hivyo TANESCO inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati ili kuhakikisha miundombinu ya umeme inaendana na kasi hiyo ya maendeleo,” amesema Twange.
Ameeleza kuwa Mradi huo umetekelezwa na kampuni za State Grid Electrical & Technical Works Limited, Central Electricals International Limited na Ezeetec Limited chini ya usimamizi wa TANESCO.
Uzinduzi wa miundombinu hiyo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha Gridi ya Taifa na kuongeza uhakika wa nishati kwa maelfu ya wananchi, taasisi za umma, wafanyabiashara na wawekezaji katika Mkoa wa Dodoma na maeneo ya jirani.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, ameipongeza TANESCO kwa utekelezaji wa mradi huo, akisema umekuwa jawabu la changamoto zilizokuwa zikitajwa mara kwa mara bungeni.
“Maswali mengi bungeni yalikuwa yanatokana na changamoto za umeme katika eneo hili. Leo tunaona majibu yake kupitia mradi huu mkubwa ambao utaimarisha maendeleo ya wananchi na wawekezaji,” amesema Mgalu.
Kukamilika kwa mradi huo kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika katika ukanda wa kati wa Tanzania, huku wananchi wakitarajia kushuhudia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya kijamii yaliyokuwa yakikwamishwa na changamoto za umeme kwa muda mrefu.





























