Home Kitaifa LONDO AHAMASISHA WANANCHI KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA...

LONDO AHAMASISHA WANANCHI KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA KWENYE NANENANE

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo,akizungumza na waandishi wa habari leo Agosti 7,2026 mara baada ya kutembelea mabanda ya Taasisi zilizochini ya Wizara ya Viwanda na Biashara wakati wa  Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane yanayoendelea viwanja vya Dkt.John Malecela Nzuguni Jijini Dodoma.

Na Alex Sonna, Dodoma

Mkakati wa Serikali wa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kupitia viwanda umeelezwa kuwa ndiyo nguzo ya kujenga uchumi shindani, kuongeza kipato cha wazalishaji na kufungua fursa zaidi za ajira kwa Watanzania.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati huo kwa kushirikiana na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuhakikisha mazao yanayozalishwa nchini yanachakatwa, yanaongezewa thamani na kuingia sokoni kama bidhaa zenye ubora na ushindani.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane,Mhe. Londo amesema mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ni malighafi muhimu kwa maendeleo ya viwanda, hivyo Serikali imeweka mazingira yatakayowezesha mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji, uchakataji hadi masoko ya ndani na nje ya nchi kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema taasisi za wizara hiyo, zikiwemo BRELA, TBS, Tume ya Ushindani (FCC),Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB),SIDO na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), zinaendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutoa elimu, usajili wa biashara, viwango vya ubora na huduma nyingine zinazolenga kuwajengea uwezo wazalishaji na wafanyabiashara kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda.

Aidha, amesema Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuwekeza katika barabara, madaraja, vivuko, umeme wa REA na miundombinu ya mawasiliano ili kupunguza gharama za uzalishaji, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuwapa wananchi taarifa sahihi za masoko zinazowaongezea tija.

Mhe.Londo amewataka wananchi kutembelea banda la Wizara ya Viwanda na Biashara katika maonesho hayo ili kupata elimu na huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi zake, akisisitiza kuwa kuongeza thamani ya mazao ndiyo njia ya kuimarisha viwanda vya ndani, kuongeza mapato ya wananchi na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uzalishaji wa bidhaa zenye ushindani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!