
Na Magrethy Katengu—Mzawa Media
Dar es Salaam
Mtandao wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni Tanzania (MMASUTA), kupitia kikundi chake cha Sanaa za Maigizo kinachoitwa Kazi Iendelee na Mama Samia, wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwashika mkono katika shughuli zote za kichama, kwa kuwapa nafasi ya kutangaza miradi iliyotekelezwa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam tarehe 1 Machi 2025, Dkt. David Msuya, ambaye ni Mwenyekiti wa MMASUTA, alisema kuwa kikundi hicho kinajumuisha wasanii wachanga ambao tayari wameshiriki katika shughuli nyingi za kuiunga mkono Serikali katika mikoa mbalimbali, ikiwemo kufanya usafi katika maeneo ya Zahanati, sehemu za miundombinu ya afya zilizojengwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.
“Mara kadhaa tunapopata nafasi, tunafanya shughuli mbalimbali za kuiunga mkono Serikali, ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika Zahanati ambazo ni sehemu ya miundombinu ya afya iliyojengwa na Serikali yetu. Kwa kuwa tuna uzoefu huo, tunamuomba Mama yetu atushike mkono ili tuwe sehemu ya kutangaza miradi iliyotekelezwa chini ya uongozi wake, kupitia sanaa yetu ya uigizaji, mashairi na nyimbo,” alisema Dkt. Msuya.

Dkt. Msuya aliongeza kuwa wakati wa mafuriko yaliyotokea wilayani Kilosa, mkoani Morogoro, kikundi hicho kilishiriki katika shughuli za kibinadamu, na hivyo wanaamini kuwa watakapopata nafasi ya kujumuika katika mikutano ya kiserikali na kichama, wataweza kutangaza vyema mafanikio ya miradi iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
“Wasanii mnaowaona hapa leo wana vipaji mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uchezaji wa ngoma za asili, uigizaji, utunzi wa mashairi, ngonjera na maigizo. Hivyo, tukishirikishwa ipasavyo katika kazi mbalimbali za Serikali, tutawawezesha wananchi kuzifahamu vyema miradi hii,” alisema Dkt. Msuya.

Aidha, Dkt. Msuya alisisitiza kuwa wasanii hao wanaimani na viongozi wa CCM, wakiwemo Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla.
Wasanii hao chipukizi wamesema kuwa wamekaa na kutafakari, na wameamua kumuomba Rais Samia kuwawezeshe kujiunga katika timu ya kushiriki katika majukwaa ya kiserikali na kichama, ili kutangaza kazi zilizotekelezwa na Serikali na kuwafikia wananchi kwa njia bora.
“Hapa kuna wasanii wenye vipaji vikubwa sana. Ikiwa itampendeza Rais Samia, tunamuomba atupe nafasi ya kutoa burudani katika ziara zake za kikazi kabla ya mikutano kuanza,” alisema Dkt. Msuya.
Zainabu Jaha, ambaye ni Katibu Msaidizi, alisema kuwa ikiwa watapewa nafasi hiyo, watafanya kazi tofauti kupitia uigizaji na ngonjera zinazozungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa Zahanati nchi nzima, na ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere.