Home Kitaifa MAWAZIRI PITIENI UPYA MIKATABA – MAJALIWA

MAWAZIRI PITIENI UPYA MIKATABA – MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Mawaziri wapitie upya mikataba ambayo nchi kupitia wizara zao zimeingia na nchi mbalimbali kwenye sekta zao ili kubaini maeneo ambayo yanahitaji kukamilishwa na kufanyiwa kazi.

Amesema ni muhimu Wizara zenye majadiliano ya mikataba na nchi nyingine zizingatie umuhimu wa majadiliano hayo na kutumia wataalamu wenye uzoefu kwenye maeneo hayo.

Amesema hayo leo (Ijumaa, Agosti 12, 2022) wakati akifunga kikao kazi cha Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu wao, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI, izingatie maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kuwa Halmashauri zote nchini zinakuwa na makadirio stahiki katika malengo ya ukusanyaji wa mapato katika mwaka ujao wa fedha sambamba na kuimarisha na kuibua vyanzo vipya vya mapato.

Tusijivunie tu kukusanya asilimia mia moja wakati tumekadiria mapato kidogo na kuna fursa ya kukusanya zaidi, mabaraza ya madiwani na watendaji wetu wafanye mapitio ya maeneo yote ya makusanyo kuona eneo hilo kwa mwezi wanakusanya kiasi gani na kujiridhisha kama ndiyo mapato halisi yanayokusanywa.”

Aidha, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango ifanye uchambuzi wa Mpango wa kuikwamua Afrika Kiuchumi, hususani Tanzania na kuainisha fursa zilizopo na iweke mikakati ya kuzitumia.

Suala hili lifanywe kwa haraka kwani mwelekeo wa Mheshimiwa Rais kwenye suala la uchumi hasa wa kilimo ni kuwachochea Watanzania kujikwamua kiuchumi. Tusipoteze fursa hii kama ina tija kwa nchi,” amesisitiza.

Kadhalika ameziagiza Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakutane na kujadili kwa pamoja mwingiliano wa kisheria kuhusu suala la uhakiki wa uthamini wa fidia wanazopaswa kulipwa wananchi baada ya Mthamini Mkuu wa Serikali kufanya uthamini wa maeneo yanayopaswa kulipwa fidia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!