Na Neema Kandoro Mwanza
MAADILI mema kwa wanafunzi yanapaswa kujengwa katika ngazi ya familia na shuleni ili tuwe na taifa lenye kuheshimu misingi ya utamaduni wetu.
Wito huo umetolewa leo kwenye mahafali ya 13 kwa darasa la saba katika shule ya awali na msingi Nyamuge Jijini Mwanza na wadau wa elimu wakisema ushirikiano huo kwa pamoja ni mhimu kumfanya mwanafunzi kuwa na maadili mema nchini.

Askofu Robert Bundala wa Kanisa la TGC alisema kutokana na kuwepo kwa mmomonyoko wa maadili hapa nchini umefika muda wa kuchukua hatua kwa pamoja kama jamii kuhakikisha kuwa watoto wa Kitanzania wanakuwa na mapenzi ya utamaduni wao.
Alisema kuwa kumuacha mtoto afanye mambo ambayo mzazi, mwalimu au mlezi wake hajui ni kosa kwani anaweza kujifunza vitu visivyo vizuri na hivyo kusababisha kuwa na tabia mbaya ndani ya jamii.
Meneja wa shule hiyo Peter Charles aliwataka wazazi kutowaruhusu watoto kuangalia filamu ambazo hawazijui kwani zingine ni mbaya hazina maadili mema.
“Sisi tumekuwa tunawafundisha wanafunzi wetu kumcha mwenyezi Mungu kwani mtoto anapokuwa na hofu ya Mungu ndo ujenzi wa maadili mema kwake”alisema Charles.
Mkurugenzi wa shule hiyo Floriana Mushi alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wanakuwa na maadili mema wanawafundisha mafunzo ya usikauti wawe na uzalendo wa kupenda nchi yao.
Mzazi wa Fahad John aliyehitimu darasa la saba John Zengo alisema anashukuru mwanaye kuwa na tabia nzuri vilevile kujengewa msingi mzuri wa Kitaaluma ambao utamfanya kumudu vizuri masomo ya sekondari.
“Tunashukuru shule hii kuwa na usikivu kwenye mambo yote ya kuwahudumia watoto wetu hivyo kutufanya wazazi tufurahie huduma wanazotoa” alisema Zengo.
Naye mzazi wa Victor Charles aliyehitimu Eliwaza Paul alishukuru namna shule hiyo inavyowaandaa watoto na kuwa na maadili mema kwenye jamii.
Alisema mchango huo wa shule ni mhimu katika kujenga jamii itakayokuwa na upendo mkubwa kwa utamaduni wao.









