Na. Neema Kandoro Mwanza
WAKULIMA wa zao la pamba nchini wamesisitizwa juu ya umuhimu wa kuzingatia usafi kwenye mnyororo mzima wa kilimo hicho kuwezesha kupatikana kwa ubora ili wapate bei nzuri ndani na nje ya nchi.
Hayo yamebainishwa jana kwenye kilele cha maonesho ya Nane nane Kanda ya Ziwa Magharibi Jijini Mwanza na Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi Bodi ya Pamba Tanzania James Shimbe.
Alisema pamba safi ambayo TCB inaiweka kwenye kundi la Tan ni nzuri na ina soko kubwa kwenye mataifa yote hapa duniani hivyo ili mkulima aweze kupata ni lazima ahakikishe kuwa kuanzia anapolima hadi kuvuna inakuwa na usafi wa hali ya juu
Shimbe alisema kuwa kulima kwa kuzingatia upandaji unaoshauliwa kitaalamu wa miche 44,444 kwenye ekari moja, kutumia mbolea za samadi na za viwandani pamoja na unyunyiziaji wa dawa itawezesha kupatikana kwa mazao mengi na yenye usafi unaotakiwa.
Naye Makaguzi wa Bodi ya Pamba Tanzania Daniel Shimbe alisema kwa sasa kumepatikana ndege ya kutotumia rubani ambayo wakulima wenye mashamba makubwa wanaweza kutumia kwa ajili ya kupulizia mashamba yao hivyo kuwawezesha kupata pamba safi yenye soko kubwa.
Alisema TCB inafanya kila jitihada kuwafikia wakulima wa zaoa hilo ili kuwapa elimu itakayowawezesha kupata mavuno mengi kwenye mashamba yao.
Mkulima toka Katoro mkoani Geita Edward Daudi alisema kuwa utoaji wa elimu unaofanywa na bodi ya pamba inawafanya waweze kupata mazao mengi kwenye mashamba yao.
Aliomba vilevile wasaidiwe kuweza kupata zana bora za kuwezesha mafanikio kwenye kilimo chao.








