MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeanza mchakato wa kupitia upya bei za Gesi Asilia Iliyokandamizwa (CNG) inayotumika kwenye magari, baada ya kubainika kuwa viwango vya sasa vimeendelea kutumika kwa takribani miaka 15 bila kufanyiwa marekebisho.

Mapitio hayo yanalenga kuhakikisha bei za gesi hiyo zinaendana na gharama halisi za uendeshaji, viwango vya faida kwa watoa huduma pamoja na uwezo wa wananchi kumudu gharama za nishati hiyo.
Hatua hiyo pia inazingatia mabadiliko ya gharama katika mnyororo mzima wa huduma, ikiwemo uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi na usambazaji wa gesi asilia.
Akizungumza Leo Novemba, 23 2026 jijini Dar es Salaam katika semina ya wadau kuhusu usalama wa matumizi ya Gesi Asilia Iliyokandamizwa (CNG), Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Lorivii Lon’gidu, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Salum Mnuna, amesema EWURA imeanza kukusanya maoni ya wadau kuhusu mapendekezo ya viwango vya faida na bei kikomo za CNG.
“Tunapenda kuona maoni yenu na ushauri wenu kuhusu mapendekezo ya viwango vya faida na bei kikomo za CNG, ili sisi kama wadhibiti tuyazingatie na kuhakikisha shughuli hizi zinafanikiwa kwa njia salama zaidi,” amesema.
Amesema ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha maamuzi yatakayofikiwa yanazingatia maslahi ya pande zote, zikiwemo za wawekezaji, watoa huduma na wananchi wanaotumia nishati hiyo.
Gharama za usafirishaji kuzingatiwa
Kwa upande wake, Meneja Mitambo Gesi Asilia(CNG)wa EWURA, Selemani Chombo, alisema mapitio hayo yanazingatia gharama za uendeshaji, mabadiliko ya thamani ya fedha za kigeni pamoja na gharama za kusafirisha gesi hiyo kutoka kwenye vyanzo vya uzalishaji hadi maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kwa sasa kilo moja ya CNG inauzwa kwa Shilingi, 1550 jijini Dar es Salaam, lakini ongezeko la matumizi ya nishati hiyo na upanuzi wa huduma katika maeneo ya Morogoro, Kibaha, Mtwara na Ruvuma vimeongeza umuhimu wa kuwa na mfumo wa bei unaozingatia gharama halisi za utoaji wa huduma katika kila eneo.
Amefafanua kuwa umbali kutoka kwenye chanzo cha gesi pamoja na gharama za usafirishaji ni miongoni mwa sababu zinazoweza kuathiri bei ya mwisho kwa mtumiaji, na hivyo kusababisha tofauti ya bei kati ya eneo moja na jingine.
“EWURA itazingatia sheria na kanuni zilizopo katika mchakato huu, huku wazalishaji, watoa huduma na watumiaji wakipewa nafasi ya kutoa maoni kabla ya viwango vipya vya bei kutangazwa na kuanza kutumika rasmi,” amesema.
Ameongeza kuwa lengo ni kuweka uwiano kati ya maslahi ya wafanyabiashara na watumiaji, ili wawekezaji waweze kuendesha shughuli zao kwa uendelevu huku wananchi wakiendelea kupata huduma hiyo kwa gharama wanazoweza kumudu.
Wawekezaji wataka uwazi wa mfumo wa bei
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Tembo Energies Limited, Prasanna Kumar, amesema matumizi ya gesi asilia kwenye magari yamekuwa msaada kwa wananchi, hasa katika kipindi ambacho bei za petroli na dizeli zinakabiliwa na mabadiliko yanayochangiwa na changamoto za uchumi wa dunia na migogoro ya kimataifa.
Amesema kampuni hiyo, ambayo ni ya kwanza inayomilikiwa na Watanzania kuendesha kituo mama cha gesi asilia, imekuwa ikihudumia wananchi jijini Dar es Salaam kwa takribani miezi 26, huku katika nyakati za mahitaji makubwa ikiweza kuhudumia zaidi ya magari 1,000 kwa siku.

“Licha ya uwekezaji mkubwa unaohitajika katika sekta hii na viwango vidogo vya faida kwa waendeshaji, anaunga mkono kuendelea kuwepo kwa bei tulivu ili kuhamasisha wananchi wengi zaidi kuachana na matumizi ya nishati zenye gharama kubwa na kutumia CNG,” amesema.
Amesisitiza kuwa umuhimu wa Serikali kuweka uwazi katika mfumo wa kupanga na kutoza bei za gesi, akipendekeza mikataba na malipo ya gesi yafanyike moja kwa moja kwa shilingi za Tanzania badala ya kutegemea thamani ya Dola za Marekani.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uwazi na kuwawezesha watumiaji kuelewa kwa urahisi gharama halisi wanazolipia.
Kuhusu mipango ya kupanua huduma, Kumar alisema Tembo Energies inaandaa mradi wa kituo kidogo cha gesi asilia iliyoyeyushwa mkoani Mtwara, utakaosaidia kusambaza nishati hiyo katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Mbeya.
EWURA yaongeza elimu ya usalama
Naye Mkaguzi wa Masuala ya Usalama wa Gesi Asilia, Baraka Majengo, alisema semina zinazoandaliwa na EWURA zina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wadau kuhusu ubora na usalama wa matumizi ya gesi asilia.
Amesema elimu hiyo ni muhimu zaidi kwa kuwa gesi hiyo inatumika kwenye magari yanayosafirisha abiria, hivyo kuzingatia viwango vya usalama ni jambo la msingi katika kulinda maisha ya watumiaji wa huduma hizo na wananchi kwa ujumla.









