Marekani yavutiwa kuwekeza Madini Mkakati Tanzania
Naibu Waziri asema Tanzania mahali salama pa uwekezaji
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amekutana na kuzungumza na Ujumbe kutoka Marekani uliongozwa na Naibu Waziri wa Nishati wa Nchi hiyo Joshua Volz ambapo pia ameambatana na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati ya Marekani pamoja na viongozi waandamizi wa Ofisi ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.
Kikao hicho, kimefanyika leo Machi 27, 2024 katika Ofisi Ndogo Wizara hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Akizunguza katika kikao hicho, Dkt. Kiruswa amesema Tanzania ni sehemu sahihi na salama ya Uwekezaji hususan katika Sekta ya Madini ambapo ameueleza ujumbe huo kuwa Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda wawekezaji ili kuongeza tija katika maendeleo ya taifa.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesema mpaka sasa nchi ya Tanzania imefanyiwa utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia ndege (high resolution airborne geophysical survey) kwa asilimia 16 pekee hivyo bado umuhimu na uhitaji mkubwa kufanyika tafiti zaidi Ili kuongeza wigo wa maeneo zaidi yatakayo pelekea kufunguliwa kwa miradi mipya ya uchimbaji madini.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa amesema Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linawalea wachimbaji wadogo wa madini kwa kuwapa mafunzo na kuwasaidia kufanya tafiti ili kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati wa Marekani Joshua Volz ameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania
katika kufanya tafiti zaidi ili kubaini maeneo mapya yenye viashiria vya madini.
Pia, Volt amesema lengo la ziara yake ni kuona jinsi gani Serikali ya Marekani inaweza kushirikiana na Tanzania katika uzalishaji wa madini Mkakati ili kusaidia uzalishaji wa Nishati safi kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira.
Volt amesema Dunia ya sasa inauhitaji mkubwa wa Madini Mkakati ambapo Serikali ya Marekani ni mdau mkubwa katika uzalishaji na utafiti wa madini hayo kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa Nishati inayoweza kusababisha hewa ya Ukaa