Home Kitaifa DIT WAWAFIKIA WAZALISHAJI WA VIATU KANDA YA ZIWA , WAJENGEWA UWEZO.

DIT WAWAFIKIA WAZALISHAJI WA VIATU KANDA YA ZIWA , WAJENGEWA UWEZO.

Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza kwa kushirikiana na Kituo cha Biashara cha Kimataifa (ITC) kupitia mradi wa MARKUP II, imeanza mafunzo ya siku tano ya utengenezaji wa viatu kwa wajasiriamali wa bidhaa za ngozi kutoka Kanda ya Ziwa, yakilenga kuwajengea uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza thamani katika mazao ya ngozi.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mratibu wa Kitaifa wa mradi wa kuongeza thamani katika mazao ya kimkakati, Bw. Safari Fungo, amesema mpango huo unalenga kuiwezesha sekta ya ngozi kuwa chachu ya ajira na maendeleo ya viwanda nchini.

“Kupitia mafunzo haya tunalenga kuwajengea wajasiriamali ujuzi wa kuongeza thamani katika mazao ya ngozi ili bidhaa zao ziwe na ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na kimataifa,” amesema Bw. Fungo.

Kwa upande wake, Afisa Dawati la Ngozi kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Gevaronge Myombe, amesema sekta ya ngozi ni mnyororo muhimu wa thamani unaoajiri watu wengi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa viwanda.

“Serikali imeipa sekta ya ngozi kipaumbele katika Sera Mpya ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya mwaka 2025 kwa sababu ina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira na kukuza uchumi,” amesema Bw. Myombe.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa DIT Kampasi ya Mwanza, Bw. William Lohay, amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza ujuzi na ubunifu katika sekta ya ngozi.

“Tunatarajia washiriki wa mafunzo haya watapata maarifa ya kisasa yatakayowawezesha kuzalisha bidhaa bora za ngozi zenye uwezo wa kushindana katika soko la kimataifa,” amesema Bw. Lohay.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Diwani wa Kata ya Ilemela, Bi. Grace Kweka, kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Ilemela,Bw.Kafiti Kafiti huku yakifundishwa na mkufunzi wa kimataifa kutoka Ethiopia.

Baadhi ya washiriki, akiwemo Bw. Joseph Papily na Bi. Joyce Dekason, wamesema wanatarajia mafunzo hayo kuwasaidia kuboresha ubora wa bidhaa zao na kupanua masoko.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!