
Na Boniface Gideon, TANGA
Katika kupambana na kutokomeza uvuvi haramu baharini pamoja na uharibifu wa rasilimali za bahari,
Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania kwa kushirikiana na GIZ chini ya mradi wa Pwani Yetu unaodhaminiwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), wamekabidhi boti ya doria kwa wavuvi kutoka eneo la Mwambani jijini Tanga kwa ajili ya kuongeza ulinzi na kutokomeza uvuvi haramu.

Boti hiyo yenye thamani ya Mil. 41 imekabidhiwa jana jijini Tanga katika jumuiya ya utunzaji wa mazingira ya baharini ‘CMA MWAKIMAM MWAMBANI’ ikiwa ni mkakati wa kutokomeza uvuvi haramu mkoani Tanga.
Akikabidhi boti hiyo, Mratibu wa Mkoa wa Tanga kutoka Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, Ahmed Salim, alisema uvuvi haramu baharini pamoja na uharibifu wa mazingira ya bahari umeleta athari kubwa kwa viumbe wa majini pamoja na matokeo hasi ya uvuvi kwa wavuvi.
“Uvuvi haramu baharini pamoja na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa mikoko na uchafuzi wa fukwe kumeleta athari kubwa sana kwa jamii, ikiwemo kushuka kwa uzalishaji wa samaki. Hivyo tunaamini kabisa boti hii itasaidia sana harakati za kutokomeza uvuvi haramu na uharibifu wa rasilimali za pwani,” aliongeza Ahmed.
Akipokea boti hiyo kwa niaba ya wananchi, Katibu Tawala wa Wilaya ya Tanga, Anjela Mono, aliwashukuru wadau wa maendeleo kwa msaada huo na kuwataka wavuvi na wakazi wa Mwambani kutunza mazingira kwa faida ya vizazi vijavyo.
“Boti hii ilitakiwa itolewe na Serikali, lakini wenzetu wamejitolea kuisaidia Serikali. Niwaombe ndugu zangu, nendeni mkaitumie kwenye malengo yaliyokusudiwa. Tunatarajia kuona mabadiliko makubwa zaidi baada ya ujio wa boti hii,” alisisitiza Anjela.








