Bodi ya Nishati Vijijini (REB) leo Mei 10, 2026 imefanya ziara katika Kampuni zinazozalisha, kusambaza bidhaa za nishati safi ya kupikia katika Mkoa wa Arusha.
Bodi hiyo ikiwa imeongozwa na Mwenyekiti wake, Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu pamoja na Wajumbe wa Bodi hiyo, Mhe. Radhia Msuya na Mhandisi Sophia Mgonja waliweza kutembelea kampuni ya Ignate Energy Access yenye bidhaa za My Sol pamoja na kampuni ya HannyG Investment.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti Kingu, amezipongeza kampuni hizo kwa kuunga mkono kampeni ya Serikali ya Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanza kutengeneza pamoja na kusambaza bidhaa za nishati safi ya kupikia huku akitoa wito kwa makampuni mengine kuendelea kuunga mkono kampeni hiyo ili malengo yaliyowekwa ya ifikapo 2034, Asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
Awali akitoa taarifa ya utendaji wa kampuni ya My Sol, Meneja Uendeshaji wa Mitambo, Joe Chambua, amesema kuwa pamoja na huduma zingine zinatolewa na kampuni hiyo ikiwamo huduma ya ufungaji wa umeme jua, kampuni hiyo imeanza kutekeleza mradi wa nishati safi ya kupikia kwa kuja na teknolojia rahisi na ya gharama nafuu ya mtambo wa biogasi.
Amesema kuwa wamefanikiwa kufunga mitambo ya biogasi katika taasisi mbalimbali nchini ikiwemo Magereza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa kampuni ya Hanny G Investment, Hanny Mbaria, ambao wanajishughulisha na utengenezaji wa majiko banifu pamoja na mkaa mbadala ameishukuru Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuipa kampuni hiyo kazi ya kusambaza majiko banifu na mkaa mbadala katika shule 53 Tanzania Bara.
Mbaria amesema licha ya mradi wa nishati safi ya kupikia kulinda mazingira lakini pia mradi huo umetoa ajira kwa vijana wengi.
“Kwa sasa kampuni yetu imekua zaidi na tumeajiri vijana wengi zaidi tofauti na hapo awali. Kwa sasa tuna wafanyakazi zaidi ya 120 wenye ajira za kudumu na wasio na ajira za moja kwa moja ni 1000,” amesema Mbaria.
















