Na Shomari Binda-Musoma
MAONYESHO ya kilimo mseto ya shirika la Vi-Agroforestry yanayofanyika kila mwaka mjini Musoma yanafunguliwa kesho kwenye kituo cha kilimo mseto kilichopo Bweri.
Shughuli za maonyesho hayo zinaendana na maadhimisho ya miaka 40 ya shirika hilo tangu lianze kufanya shughuli zake za kilimo hapa nchini.
Katibu mkuu Wizara ya kilimo na mifugo Profesa Riziki Shekimweri anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo.
Mmoja wa waratibu wa maonyesho hayo kutoka AICT, Davis Dominick amesema maandalizi yote yamekamilika tayari kwa ufunguzi.
Amesema tayari vikundi vya wakulima kutoka ndani na nje ya mkoa wa Mara vimeshawasili kwenye viwanja vya maonyesho.
Davis amesema kwenye maonyesho ya mwaka huu licha ya maonyesho ya shughuli za wakulima lakini mafunzo na elimu ya kilimo chenye tija itatolewa kwa wakulima.
“Maandalizi yanakwenda vizuri kwa ajili ya uzinduzi wa kesho na tayari baadhi ya wakulima wameshafika viwanja vya maonyesho kuonyesha shughuli zao”
“Tunawaomba wananchi kufika kwenye kituo cha mafunzo ya kilimo mseto pale Bweri ili waweze kujifunza na kujionea bidhaa mbalimbali za wakulima” amesema Davis.
Kwa upande wao wakulima ambao tayari wameshafika viwanja vya maonyesho hayo wamesema mwaka huu wanataraji kujifunza mambo mapya na kuonyesha bidhaa zenye ubora.








