Na Neema Kandoro, Mwanza
SERIKALI imepunguza gharama zilizokuwa zikitumika kutoa hati miliki ya ardhi kwa mwaka 2023/24 ili kuwezesha watanzania wengi kumudu hivyo kupunguza migogoro iliyokuwa ikijitokeza kwa watu wengi na kupoteza muda wa uzalishaji mali.
Wito huo umetolewa kwa Mzawa Blog leo Jijini Mwanza na Kamishina wa ardhi Msaidizi Mkoani Mwanza Happiness Mtutwa akisema gharama hizo zimepunguzwa kwa kiwango cha nusu ya kiwango halisi kilichokuwa awali.
Mtutwa aliwataka watu mkoani Mwanza ambao bado hawajapata hati miliki ya viwanja vyao kuanza mchakato ili waweze kupata kwani ofisi yao inafanya kazi kwa haraka ili kuwezesha watanzania kufanya shughuli za maendeleo.
Alisema kwa sasa migogoro iliyopo ni baina ya watu wanaopakana kuingiliana na hivyo kuanza mvutano wa wao kwa wao na hivyo kuonekana kuna matatizo ambayo yanahusisha idara ya ardhi.
“Jukumu la kulinda ardhi baada ya kupimwa ni la mwananchi mwenyewe hivyo kunapokuwa na kuingiliwa kwa mtu na jirani yake hilo ni tatizo la kosa la kijinai ambalo linaweza kupelekwa mahakani” alisema Mtutwa.
Alisema kupatikana kwa hati miliki kunamwezesha mtu kuwa na dhamana ya mali isiyohamishika ambayo itamwezesha kutumia kupata mikopo kwenye taasisi za fedha anapokuwa na uhitaji.
Mtutwa alisema ofisi yake inaendelea kutoa elimu hiyo katika mitaa mbalimbali jijini Mwanza na Kwenye maeneo mengine wilayani ili kuwezesha watu wengi kupata fursa ya kupima maeneo yao na kupata hati miliki.








