Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za bima ya afya, huku ukisikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wanachama katika matumizi ya kadi zao za bima ya afya.
Huduma hizo zinaendelea kutolewa kupitia banda la NHIF katika maonesho maalumu ya kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo, yanayofanyika katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma. Katika maonesho hayo, wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kupata ufafanuzi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na NHIF.
Kupitia maonesho hayo, wananchi wanapata fursa ya kuwasilisha changamoto zinazohusiana na matumizi ya kadi za bima ya afya, kupata ufumbuzi wa changamoto hizo pamoja na kuelekezwa taratibu za kupata na kutumia huduma za bima ya afya kwa usahihi.
Aidha, NHIF inatumia maadhimisho hayo kama jukwaa la kuimarisha uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa kuwa na bima ya afya, manufaa ya huduma za Mfuko na umuhimu wa wananchi kujiunga na mifumo ya bima ya afya ili kupata uhakika wa huduma wanapozihitaji.
Maonesho hayo ni sehemu ya juhudi za NHIF za kusogeza huduma karibu na wananchi, kuimarisha uhusiano na wanachama pamoja na kuendelea kutekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kupitia mifumo ya bima ya afya.










