
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura amewataka askari kuendelea kujifunza na kujiimarisha katika mbinu mbalimbali za kiutendaji ili kukabiliana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia, yanayoendelea kubadilisha mbinu za uhalifu na hivyo kuimarisha mapambano dhidi ya wahalifu.
IGP Wambura ameyasema hayo Novemba 25, 2026 wakati akifunga rasmi mafunzo ya Wakufunzi wa Polisi (Basic Instructor Course) yaliyofanyika Shule ya Polisi Tanzania, Kambi ya Kamba Pori, iliyopo Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.


Amesema kuwa, uhalifu unabadilika kwa kasi na wahalifu wameendelea kubuni mbinu mpya na baadhi ya matukio ya uhalifu yanahitaji maandalizi, utaalamu vifaa na uwezo maalum ya kuyakabili.

Naye Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu, CP Tatu Jumbe amesema, kupitia mafunzo hayo Jeshi la Polisi litakuwa na kundi la wakufunzi watakaosaidia kuimarisha ubora wa Mafunzo na kuongeza ufanisi na kuhakikisha kuwa wanakuwa na maarifa na stadi zinazokidhi mahitaji ya sasa na ya baadae ya Jeshi la Polisi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Polisi Tanzania- Moshi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhani Mungi, amesema mafunzo waliyoyapata askari hao yanapaswa kutumika kwa kuzingatia sheria za nchi, kanuni na taratibu za Jeshi la Polisi, haki za binadamu, uwajibikaji na misingi ya matumizi halali ya lazima na yenye uwiano wa nguvu.

Mafunzo hayo yana lengo la kuwajengea uwezo askari kitaaluma, kiufundi na kiutendaji ili waweze kutekeleza majukumu ya ukufunzi kwa ufanisi zaidi katika vituo vya kazi na maeneo mengine watakayopangiwa.










