Na.Alex Sonna-DODODMA
Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) umewataka Maafisa Biashara nchini kushirikiana kwa karibu na taasisi hiyo katika kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia vipimo sahihi, hatua inayolenga kulinda maslahi ya walaji na kuimarisha uadilifu katika shughuli za biashara nchini.
Meneja wa Sehemu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa WMA, Jadi Athumani Kijumu, amesema hayo wakati wa Kikao cha Tatu cha Wizara ya Viwanda na Biashara na Maafisa Biashara wa mikoa nchini, kilichofanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo maafisa hao kuhusu majukumu ya taasisi mbalimbali katika sekta ya biashara.
Kijumu amesema WMA imetumia kikao hicho kuwaelimisha Maafisa Biashara kuhusu majukumu yake, pamoja na namna wanavyoweza kushirikiana katika kuwafikia wafanyabiashara na kuhakikisha elimu kuhusu matumizi ya vipimo sahihi inawafikia wananchi katika maeneo yote.
Amesema Maafisa Biashara ni kiungo muhimu kati ya WMA na wafanyabiashara kwa kuwa wanafahamu kwa karibu maeneo wanakofanyia shughuli zao.
“Katika utekelezaji wa majukumu ya uhakiki wa vipimo, WMA hushirikiana na Maafisa Biashara kuwaunganisha na wafanyabiashara, huku taasisi hiyo pia ikiwa mjumbe katika Kamati za Ushauri za Mikoa ambako hushirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua kero zinazohusu biashara, ushirikiano huo unarahisisha kubaini changamoto na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.”amesema Bw. Kijumu
Aidha, Kijumu amewataka Maafisa Biashara kuweka mbele ulinzi wa mlaji kwa kuhakikisha changamoto zinazohusu usalama, afya na matumizi ya vipimo zinawasilishwa kwa WMA ili hatua zichukuliwe. Amesema ushirikiano huo utasaidia kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinakaguliwa na kuthibitishwa kuwa sahihi, hivyo kumlinda mlaji dhidi ya kupunjwa.
Amesema pia Maafisa Biashara wanapaswa kushirikiana na WMA katika kutoa taarifa na takwimu sahihi kuhusu wafanyabiashara waliopo katika maeneo yao, jambo litakalowezesha taasisi hiyo kupanga na kutekeleza shughuli za ukaguzi kwa ufanisi. Ameeleza kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi ni muhimu katika kuhakikisha huduma za vipimo zinawafikia wafanyabiashara kwa wakati na kulinda maslahi ya walaji.
Kijumu amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya WMA, Maafisa Biashara na wafanyabiashara ni muhimu katika kujenga mazingira ya biashara yenye haki na uwazi, huku akiwataka Maafisa Biashara kuendelea kuwa kiungo cha kufikisha elimu na kuhakikisha vipimo vinavyotumika katika biashara vinakidhi viwango vinavyotakiwa kwa manufaa ya wafanyabiashara na walaji.


















