Home Kitaifa JAMII YAHASWA KUWAKUMBUKA WAHITAJI

JAMII YAHASWA KUWAKUMBUKA WAHITAJI

Wanachama wa AMO na DORCAS wa Kanisa la Waadventista Wasabato Ilala wamewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea na kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, wakieleza kuwa kuwahudumia wahitaji ni sehemu ya imani na wajibu wa kijamii.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada katika Kituo cha Kulelea Watoto Yatima cha Buloma Foundation, kilichopo Kibaha Picha ya Ndege, mkoani Pwani, Kiongozi wa AMO na DORCAS Ilala, Neema Matochi, amesema ziara hiyo imelenga kuwafariji watoto pamoja na kuwapatia mahitaji mbalimbali muhimu, ikiwemo vyakula, nguo na vifaa vya shule.

Matochi amewashukuru viongozi na waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato Ilala kwa ushirikiano wao uliofanikisha zoezi hilo, huku akitoa wito kwa jamii kujitokeza kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu na makundi mengine yenye uhitaji.

Kwa upande wake, mmoja wa watendaji wa Buloma Foundation, Baraka Kiando, amelishukuru Kanisa la Waadventista Wasabato Ilala kwa upendo na moyo wa kujitolea waliouonyesha kwa watoto hao, akisema msaada walioutoa umechangia kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku pamoja na mahitaji ya elimu.

Amesema kituo hicho kinahudumia watoto 69, wakiwemo wavulana 35 na wasichana 34, na hupokea misaada kutoka kwa wadau mbalimbali.

Kiando ametoa wito kwa jamii kutokujikita tu katika kutoa misaada ya vitu, bali pia kutenga muda wa kuwatembelea watoto hao, kuzungumza nao, kuwapa ushauri wa kimaadili na kiimani, pamoja na kuwafariji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kufanyia tathmini misaada inayotolewa kwa watoto kabla ya kuikabidhi, ili kuhakikisha inalenga ustawi wao na haihusiani na vitendo vinavyoweza kuhatarisha maadili yao.

Nao baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Yohana Almasi na Grepea Jeremia, wamelishukuru Kanisa la Waadventista Wasabato Ilala kwa msaada wa vifaa vya shule, wakisema umewapa hamasa na kuwawezesha kuendelea na masomo yao katika mazingira bora zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!