
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yatakayofanyika Julai 1, sambamba na utoaji wa Tuzo za Rais kwa Walipa Kodi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema kwa mara ya pili mfululizo Rais Samia atatoa tuzo hizo ikiwa ni ishara ya kuthamini mchango wa walipa kodi katika maendeleo ya taifa.
Alisema hafla hiyo itafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City na itawakutanisha walipa kodi kutoka mikoa yote 35 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mwenda alisema tuzo hizo zitatolewa kwa walipa kodi wakubwa na wadogo waliozingatia sheria za kodi, huku akibainisha kuwa lengo ni kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kutambua mchango wa wananchi katika kujenga uchumi wa nchi.
Aidha, alimpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuiwezesha TRA kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na mazingira ya biashara, hatua ambazo amesema zimechangia kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali na kuboresha huduma kwa walipa kodi.
Mwenda aliwataka Watanzania kuendelea kushiriki kikamilifu katika ulipaji wa kodi, akisisitiza kuwa kodi ndiyo msingi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma muhimu za kijamii nchini.









