Home Kitaifa ZANZIBAR KUWA KITOVU CHA UZINDUZI WA MSAADA WA KISHERIA AWAMU YA PILI

ZANZIBAR KUWA KITOVU CHA UZINDUZI WA MSAADA WA KISHERIA AWAMU YA PILI

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17,2026 jijini Dodoma  kuhusu uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria itakayofanyika Juni 20 mwaka huu, Zanzibar.

Na.Alex Sonna-DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC II) Juni 20,2026 katika Viwanja vya Maonesho Dole, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi wote.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17,2026  jijini Dodoma leo, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema  kampeni hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa huduma za msaada wa kisheria, elimu ya sheria na ushauri wa kisheria ili kuongeza uelewa wa haki na wajibu wao katika jamii.

Dkt. Homera amesema kampeni hiyo ni utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha huduma za sheria na haki zinapatikana kwa wananchi wote bila ubaguzi, hususan makundi maalumu na wananchi wa maeneo ya pembezoni ambao mara nyingi hukumbwa na changamoto za kupata huduma hizo.

Amefafanua kuwa Awamu ya Pili ya kampeni hiyo itaendelea kutumia kaulimbiu ya “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo,” ambayo inaakisi dhamira ya Serikali ya kuimarisha utawala wa sheria, usawa na maendeleo ya taifa.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mafanikio ya Awamu ya Kwanza ya kampeni iliyotekelezwa kuanzia Aprili 2023 hadi Juni 2025 ndiyo yamechochea kuanzishwa kwa awamu mpya. Katika kipindi hicho, kampeni ilitekelezwa katika mikoa yote 31 ya Tanzania Bara pamoja na mikoa yote mitano ya Zanzibar.

Amesema Zanzibar pekee, jumla ya wananchi 422,908 walinufaika na huduma mbalimbali za msaada wa kisheria, ambapo wanaume walikuwa 213,723 huku wanawake wakifikia 209,185.

“Matokeo haya yanaonesha wazi umuhimu wa kampeni hii katika kuwajengea wananchi uelewa wa sheria, haki na wajibu wao pamoja na kusaidia kutatua migogoro mbalimbali ya kisheria inayowakabili,” amesema Dkt. Homera.

Katika awamu mpya, wananchi watapata huduma zinazohusu masuala ya ndoa na talaka, mirathi, migogoro ya ardhi, haki za watoto, ukatili wa kijinsia, haki za wafanyakazi pamoja na usuluhishi wa migogoro kwa njia mbadala.

Huduma nyingine zitakazotolewa ni pamoja na usajili wa matukio muhimu ya maisha, upatikanaji wa nyaraka za utambulisho, uandaaji wa nyaraka za kisheria na utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi.

Dkt. Homera amesema maandalizi yote ya uzinduzi wa kitaifa yamekamilika na kwamba zaidi ya washiriki 15,000 wanatarajiwa kuhudhuria hafla hiyo, wakiwemo viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa dini, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia, wataalamu wa sheria na wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar.

Ameongeza kuwa sambamba na uzinduzi huo, huduma za msaada wa kisheria zitatolewa kupitia mabanda katika wilaya za Mjini, Magharibi A na Magharibi B, huku timu za wataalamu zikitembelea shehia mbalimbali kutoa elimu ya sheria, ushauri na utatuzi wa migogoro.

Waziri huyo ametumia fursa hiyo kupongeza ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utekelezaji wa kampeni hiyo, akisema ni mfano halisi wa manufaa ya Muungano katika kuwahudumia wananchi.

Aidha, amewataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uzinduzi huo na kutumia fursa ya kupata huduma mbalimbali za kisheria zitakazotolewa bila malipo.

“Ushiriki wa wananchi katika kampeni hii utasaidia kuongeza uelewa wa haki zao za kisheria, kuimarisha amani na utulivu katika jamii pamoja na kuchochea maendeleo ya Taifa,” amesema 

Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imeendelea kuwa miongoni mwa programu muhimu za Serikali zinazolenga kusogeza huduma za haki karibu na wananchi na kujenga jamii inayozingatia sheria, usawa na utawala bora.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17,2026 jijini Dodoma  kuhusu uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria itakayofanyika Juni 20 mwaka huu, Zanzibar.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17,2026 jijini Dodoma  kuhusu uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria itakayofanyika Juni 20 mwaka huu, Zanzibar.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 17,2026 jijini Dodoma  kuhusu uzinduzi wa awamu ya pili ya kampeni ya msaada wa kisheria itakayofanyika Juni 20 mwaka huu, Zanzibar.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!